WATUMISHI watatu wa Mahakama akiwemo hakimu mmoja wamepewa notisi, wakikabiliwa na tuhuma za kula rushwa.
Katibu wa Tume ya Utumishi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar, Yessaye Kayange, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari, wakati akiitambulisha uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya mahakama.
Kayange ambaye pia ni Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu, alisema kumetolewa notisi kwa watumishi hao na uchunguzi unaendelea juu ya tuhuma hizo zinazowakabili.
Bila kutaja majina ya watumishi hao Kayange, alisema hivi sasa tayari hatua zimeanza kulishughulikia suala hilo ili kuweza kupatikana ukweli halisi wa madai dhidi yao.
Alisema tuhuma hizo zinamuhusisha hakimu na karani wake, huku mfanyakazi mwengine naye akiendelea kuchunguzwa kutokana na madai hayo.
Alifahamisha katika hatua hizo hivi sasa wapo katika kuwapa nafasi watuhumiwa hao ili wajieleze na uongozi wa Mahakama uweze kuwasikiliza utetezi wao juu ya suala hilo.
Alisema baada ya kumaliza hatua hizo ndipo uongozi wa mahakama hiyo utapoweza kukaa na kuamua hatua zitakazochukuliwa dhidi yao.
Alisema adhabu hizo zitapochukuliwa ni sehemu ya Mamlaka ya Tume ya Utumishi ya Mahakama ambayo imepewa uwezo wa kuajiri, kuachisha kazi, kuongeza mishahara huku ikisimamia watumishi katika kada zote za Mahakama.
Alisema mfumo wa awali ulikuwa ukiwafaidisha ngazi za juu pekee kwa kuwawekea maslahi bora kada ya mahakimu na Majaji huku ukiacha wafanyakazi katika ngazi ya utawala.
Kadhia hiyo ya watumishi wa Mahakama kula rushwa imekuja siku chache baada ya Baraza la Wawakilishi kupitisha sheria ya rushwa.
Hivi karibuni Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Omar Othman Makungu, katika maadhimisho ya siku ya Sheria Zanzibar alieleza kuwepo kwa madai ya rushwa kwa baadhi ya wWatumishi wa Idara hiyo na kueleza kuwa suala hilo amekuwa akilifanyiakazi.
Jaji Makungu aliahidi kuwa pindipo itapobainika kuwapo kwa ukweli juu ya tatizo hilo, uongozi wa Mahakama hautasita kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi yoyote ataepatikana na hatia.
0 Comments