MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Asha Seif Iddi ametaka kuitishwa kamati ya wazee wa skuli ya Fujoni kujadili matokeo mabaya ya kidato cha nne katika skuli ya kijiji hicho.
Mke huyo wa Balozi Seif alieleza hayo huko Fujoni alipokuwa akiwatunuku vyeti wanafunzi wa skuli ya maandalizi ya Madrasa ya Dhin Noorayni, katika mahafali yaliofanyiika katika viwanja vya skuli ya Fujoni wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Alisema kamati hiyo iitishwe ili kujadili ubaya wa matokeo hayo sambamba na kuweka mikakati ya kutorejea kwa matokeo kama hayo katika skuli hiyo.
Alisema inasikitisha kuona skuli hiyo imeshinda kufaulisha wanafunzi wa kutosha ikizingatiwa kuwa ilikuwa na matokeo mazuri na kuwa skuli ya kwanza katika jimbo hilo.
Mama Asha alisema mwaka jana skuli ya Fujoni iliweza kutoa wanafunzi 16 kuingia kidato cha sita, lakini mwaka huu mwanafunzi mmoja tu ndiye aliyepata alama za kuendelea na masomo ya kidato cha tano.
Alisema kikao hicho kitapokaa kitapaswa kutafakari kwa kina tatizo hilo ikiwa pamoja na kujiridhisha na elimu inayotolewa kama inawatosheleza wanafunzi wa skuli hiyo.
“Nitaitisha kamati ya wazazi ya jimbo ili tuangalie wapi tulipokosea na tujirekebishe, kwani hali hii inatisha na nimepatwa na hofu juu ya kuwepo usimamizi mzuri kwa watoto wetu”, alisema.
Alisema kuwa ipo haja ya kubadilika kwa kutafutwa mbinu zitakazohakikisha wanafunzi hao wanafanya vizuri katika mitihani yao.
Aidha Mama Asha aliwataka wazazi kuona wanawalipia gharama za kuchangia masomo kwa watoto wao kutokana na kujitokeza tatizo la kuchelewa kulipa ada.
Hata hivyo Mama Asha aliahidi kuendeleza ushirikano na walimu na wanafunzi wa skuli za jimbo hilo ikiwa pamoja na kutoa misaada mbali mbali.
Mama Asha alichangia shillingi 500, 000 na kuahidi kutoa matofali kwa ajili yakumalizia ujenzi wa kituo cha maandalizi hiyo.
Mapema wanafunzi wa kituo hicho walileza katika risala yao licha ya kupata elimu, lakini bado wanasumbuliwa na mazingira ya sehemu wanatopata masomo yao kutokana hairidhishi kiafya ha hakiwapi utulivu wa kuzingata masomo yao.
0 Comments