6/recent/ticker-posts

Jaji Chande: Serikali Itatue Changamoto za Kimahakama

Joseph Ngilisho, Arusha

JAJI Mkuu wa Tanzania, Othman Chande ameiomba serikali kukarabati majengo ya mahakama yaliyochakaa pamoja na kuboresha huduma za kimahakama ili kuharakisha utolewaji wa haki.

Sambamba na hilo, Jaji huyo aliiomba serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuendesha shughuli za mahakama ili ziweze kusaidia katika upatikanaji wa vitendea kazi na changamoto zingine zinazozikabili mahakama.

Alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa chama cha wanasheria nchini (TLS), uliolenga kutathmini utoaji wa haki katika mahakama, majukumu ya mahakama na majukumu ya chama cha wanasheria TLS unaofanyika mjini hapa.


Alisema, majengo ya mahakama nyingi hapa nchini yamekuwa chakavu ambapo pia kumekuwepo na maeneo mengi kutokuwa na nyumba rasmi za kuendesha shughuli za mahakama huku kazi hiyo ikifanyika katika magodauni na nyumba za kukodi.

Jaji huyo alisema kumekuwepo na changamoto nyingi za kimahakama hususani mahakama za mwanzo zinazokabiliwa na upungufu mkubwa wa mahakimu, rasilimali watu, fedha na mfumo wa uendeshaji wa sheria.

Jaji Chande aliongeza kuwa, changamoto ya rasilimali watu imefanya uwiano wa kimahakama na mahakimu kuwa mkubwa, akitolea mfano kwamba hapa nchini zipo mahakama 1005 na mahakimu ni 732 hali ambayo haijitoshelezi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alifahamisha kuwa katika kila watu watu milioni moja huhudumiwa na majaji wawili na kwa nchi za magharibi Ulaya kuna majaji 50 kwa kila watu milioni moja na kuiomba serikali kupunguza uwiano uliopo.


Aidha alisema kuwa, huduma za mahakama za rufaa zimekuwa mbali kiasi kwamba pindi mwananchi anapoamua kukata rufaa humgharimu kiasi kikubwa cha fedha kuitafuta huduma hiyo na matokeo yake mwananchi asiye na uwezo kukata tamaa na kukosa haki yake.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla alisema bado wanakabiliwa na changamoto ya mfumo wa uendeshaji madai ambayo yanatakiwa kubadilishwa ili kuweza kufanikisha shughuli mbali mbali za kimahakama.

Stolla alifafanua kuwa, ni vizuri mahakama ziweke utaratibu wa kutolewa kwa mafungu ya kutosha ili waweze kufanya kazi kwa muda wa kutosha na hatimaye wananchi waweze kupata haki zao za msingi hususani za kimahakama.

Alisema kuwa, serikali itoe sera ya msaada wa sheria ili wananchi ambao hawajafikiwa waweze kufikiwa na kuzifahamu sheria mbalimbali hali itakayowawezesha kutodhulumiwa haki zao za msingi.

Post a Comment

0 Comments