6/recent/ticker-posts

Uingiaji Vifaa Chakavu Janga la Kimazingira


· Wawekezaji hawaheshimu uhifadhi wa mazingira

Na Mwashamba Juma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdul-habib Fereji amesema Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya ujenzi wa miradi ya uwekezaji isiyofuata taratibu za sheria za mazingira.

Alisema miradi 150 ilifanyiwa ukaguzi kama imefuata kanuni za mazingira katika ujenzi wake, ambapo kati ya hiyo 80 ilibainika imekengeuka kwa kutofuata kanuni za kimazingira.

Waziri huyo alieleza hayo jana ofisini kwake Mazizini alipozungumza na waandishi wa habari akieleza mafanikio na changamoto za wizara yake.


Alisema hatua zilizochukuliwa ni kwa wawekezaji hao waliokiuka taratibu za kimazingira ni kusimamishwa kwa miradi yao ya ujenzi, huku mingine ikiruhusiwa baada ya kutimiza masharti.

Waziri huyo alifahamisha kuwa wizara yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi zinazohusika na ardhi, uwekezaji na utalii ili kuhakikisha miradi inayowekezwa nchini inafuata kanuni na taratibu za kimazingira.

Alifahamisha kuwa miradi kabla ya kuwekezwa ni lazima ifanyiwe tathmini ya kimazingira, taratibu za kimazingira ili kuepuka athari mbaya ambazo zinaweza kujitokeza baada ujenzi, lakini suali hilo limekuwa na changamoto kubwa.

Katika hatua nyengine, alisema uingizaji wa bidhaa chakavu nao ni janga la kimazingira linaloinyemelea Zanzibar ambapo katika utafiti uliofanywa mwaka 2010, umebainisha kuwa wastani wa miaka sita yaliingizwa makontena 23,000 kwa mwaka.

Alisema katika utafiti huo, imebainika kwa uchache asilimia 20 ya makontena hayo yanakisiwa kuingiza bidhaa chakavu kila mwaka ambapo kwa ujazo wa kontena la futi 20 na uzito wake ni tani 21.6.

“Hesabu zinaashiria kuwa Zanzibar inaingiza kiasi cha tani 99,360 za bidhaa chakavu kwa mwaka, bidhaa hizo zinaongozwa na TV, Radio, Friji, Cookers na Freezers”, alisema waziri huyo.

Alisema Tume ya Utangazaji Zanzibar imepiga tathmini na kubaini kuwa kuna televisheni 300,000 chakavu na redio 980,000 na kwamba hakuna ufumbuzi wa kujua vipi na wapi itakapohitajika kuzitupa bidhaa hizo bila ya kuathiri mazingira ya nchi yetu.

Akizungumzia suala la mabadiliko ya tabia nchi, waziri Ferej, alisema tatizo hilo ni la kilimwengu ambapo athari zake zimeanza kuonekana wazi wazi katika sehemu kadhaa za visiwa vya Zanzibar.

Alisema mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakiathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo kutokana na kusababisha ukame au mvua kunyesha kwenye wakati usiotarajiwa.

Aidha athari nyengine ni kuongezeka ka joto baharini na kuharibika kwa matumbawe, pamoja na upungufu wa vianzio vya maji kutokana na kukosekana kwa mvua.

“Zanzibar hivi sasa tunashuhudia kuongezeka kwa kasi ya mmong’onyoko wa fukwe katika sehemu mbambali za ukanda wa pwani wa visiwa vya Unguja na Pemba, hali hii inasababisha baadhi ya nyumba na miti ya kudumu kuanguka”, alisema waziri huyo.

Akizungumzia janga la maradhi ya UKIMWI, waziri Ferej alisema pamoja na kwa kiasi kuonena Zanzibar kuweza kudhibiti maradhi hao kwa kiwango cha asilimi 0.6, bado juhudi zichukuliwe ili iweze kufikiwa zero tatu.

“Wito wa kimataifa unatutaka tuhakikishe kuwa tunafikia lengo la kuwa na ziro tatu, yaani kwanza yasiwepo maambukizi mapya, pili usiwepo unyanyapaa kwa watu wote wanaoishi na virusi vya UKIMWI na wale walio kwenye makundi maalum, na tatu visiwepo vifo vinavyotokana na maambukizi ya maradhi ya UKIMWI”, alisema.

Aidha waziri huyo alibainisha changamoto mbali mbali juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya pamoja na matatizo yanayowakabili watu wenye ulemavu.

Post a Comment

0 Comments