6/recent/ticker-posts

Kilimo Yanunua Matrekta 10

Na Mwashamba Juma

WIZARA ya Kilimo na Maliasili katika kuimarisha harakati za kilimo nchini na kwenda sambamba na dhana ya mapinduzi ya kilimo, imenunua matrekta 10 yaliyogharimu shilingi milioni 590.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Bandarini Zanzibar, Mkurugenzi wa Idara ya Kilimo, Mberik Rashid Said, alisema kutokana na uhaba wa matrekta uliopo serikali imeona ipo haja kuongeza matrekata hayo ili kukidhi mahitaji ya wakulima.


Alisema matrekta hayo yaliyonunuliwa kutoka katika kampuni ya Suma JKT Tanzania, yanatarajiwa kutumika katika shughuli za kuchimba na kuburugia mashamba ya mpunga.

Alisema kwa siku yatatumika kufanya kazi hiyo kwa zaidi ya hekta 15 kwa Unguja na Pemba, ambapo inatarajiwa Pemba kupelekwa manne na sita kubakia Unguja.

Akiyataja mabonde yatakayoburugwa na matrekta hayo Mberik, alisema kwa Unguja ni mabonde ya Cheju, Kilombero, Kama na Bopwe.

Na kwa upande wa Pemba mabonde ya Kibirinzi, Utaani, Makombeni, Micheweni, Pujini na Ole ndio yanayotarajiwa kuburugwa.

Alisema kuongezeka kwa wakulima wengi na maeneo mengi kwa ajili ya kilimo, serikali imeandaa mbegu za muda mfupi na muda mrefu ili kukidhi haja ya wakulima hao.

Hivi karibuni wizara hiyo ya Kilimo ilipokea msaada wa trekata ndogo power tiller 50 zilizogharimu dola za kimarekani 200,000 kutoka kwa ubalozi wa Iran nchini Tanzania.

Hatua ya serikali kununua matrekta hayo ni miongoni mwa juhudi za kukuza uchumi wa nchi.

Post a Comment

0 Comments