6/recent/ticker-posts

Majengo Skuli Binafsi Hayakidhi Haja - RC

Na Salum Vuai, Maelezo

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi Khamis, amekiri kuwa majengo mengi yanayotumiwa kufunguliwa skuli binafsi, hayakidhi haja.

Akijibu masuala ya waandishi wa habari katika mkutano aliowaandalia kuelezea utendaji ndani ya mkoa wake, alisema baada ya serikali kufungua milango kwa watu wanaotaka kuanzisha skuli, kumekuwa na skuli nyingi ambazo majengo yao hayatimizi vigezo vinavyotakiwa.


Katika mkutano huo uliofanyika ofisini kwake jana, Khamis alieleza kuwa, kuna mambo mengi ya kuzingatiwa kabla mtu hajapewa leseni ya kaunzisha skuli, ikiwemo mazingira ya eneo analotaka kuendesha shughuli hiyo.

Alitaja baadhi ya vigezo, kwamba ni pamoja na uwanja wa kucheza wanafunzi, na kutochanganyika na makaazi ya watu ili kuwawezesha walimu na watoto kusomesha na kusoma kwa utulivu na amani.

Aidha alifahamisha kuwa, hata ramani za majengo yenyewe lazima ziwe zimekusudiwa kwa ajili ya skuli tangu awali, badala ya mtindo uliopo sasa, ambapo watu wengi huzigeuza nyumba zao za kuishi kuwa skuli hasa za maandalizi na msingi.

Alisisitiza umuhimu wa watu wanaotaka kuanzisha skuli kufuata taratibu na kuhakikisha majengo yao yanakaguliwa na Idara yenye dhamana ili yaweze kuwawekea wanafunzi na walimu mazingira yanayofaa.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na tatizo hilo, Ofisa Elimu Mkoa wa Mjini Magharibi Maalim Yahya Ilyaas, alisema kimsingi mtu anayetaka kufungua skuli, hulazimika kuandika maombi, na baadae Bodi ya wizara inapeleka wakaguzi kwenye kwa ajili ya kukagua jengo, na pia kutoa maelekezo ya namna linavyotakiwa liwe.

Hata hivyo, alieleza kuwa, kwa vile mara nyingi baadhi ya majengo yanakuwa na mapungufu, muombaji hupewa kibali cha muda huku suala lake likiwa chini ya Mrajis ambaye ndiye anayepaswa kutoa vibali, akitakiwa atimize masharti kabla kupewa leseni ya kudumu.

Mkuu wa Mkoa aliahidi kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na maofisa wa Elimu pamoja na wizara kwa jumla, wataendelea kuzifanyia ukaguzi skuli hizo, ili kuhakikisha zinafikia vigezo vilivyowekwa.

Kuhusu mazingira mabaya yaliyopo skuli ya Vikokotoni ambayo imekuwa kero kubwa kwa wanafunzi na walimu, Mkuu wa Mkoa alikiri kuwepo kwa hali hiyo, lakini akasema kuwa ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mjini inaandaa utaratibu mzuri ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Alitoa mfano wa wafanyabiashara waliokuweko pembezoni mwa skuli ya Darajani ambao sasa wamehamishiwa Saateni ambayo sasa utulivu umerudi, lakini akaeleza kuwa mpango wa kuwahamisha wale wa Vikokotoni hauwezi kufanywa kwa kukurupuka bila maandalizi ya kutosha kuwatafutia eneo mbadala.

Post a Comment

0 Comments