KAMPUNI 100 za kilimo cha nafaka kutoka nchi mbali mbali barani Afrika zinatarajiwa kushiriki maonesho ya kilimo na biashara yatakayofanyika jijini Arusha.
Maonesho hayo yatalenga zaidi kutoa mafunzo kwa wakulima, kuhusu kilimo, biashara na kuweza kuonyesha ni jinsi gani wakulima hao wataweza kunufaika zaidi na mazao yao na jinsi ya kuweza kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa baraza la nafaka la kanda ya Afrika Mashariki (EAGC), Gerald Masika aliyasema hayo katika uzinduzi wa maonyesho ya kilimo biashara yatakayofanyika jijini Arusha.
Masika aliongeza kuwa maonyesho hayo yanaandaliwa na EAGC kwa kushirikiana na kituo cha utafiti wa kilimo cha Selian (SARI) kilichopo Ngaramtoni ya chini jijini Arusha na yatafanyika katika kituo hicho cha utafiti.
Alisema kuwa, maandalizi ya maonyesho hayo yanatarajiwa kugharimu kiasi cha dola za kimarekani 80,000 hadi 90,000 ambapo mkulima amepewa kipaumbele zaidi kushiriki kikamilifu kutokana na umuhimu wa biashara ya kilimo na mazao.
Alifafanua kuwa, maonyesho hayo yatasaidia kupata utatuzi wa changamoto zinayowakabili wakulima ikiwa ni pamoja na kukabiliana na tatizo la mbegu feki zinazoingizwa kwenye mzunguko wa biashara za mbegu na mawakala wa pembejeo.
Aidha aliongeza kuwa wakulima nchini watajifunza njia za kukabiliana na soko la mazao kufutaia serikali kuzuia zoezi la uvushwaji wa mazao mbalimbali hususani mahindi nje ya nchi kwani changamoto hiyo imewafanya wakulima wakate tamaa ya kulima na wengine kuishia kupata kupata hasara.
Naye Mkurugenzi wa EAGC nchini, David Tuhoye aliwataka wakulima nchini kujitokeza kwa wingi katika kushiriki maonyesho hayo ili waweze kujifunza uzoefu kutoka kwa wenzao.
Aidha alisema kuwa, kwa sasa wakulima kwa hapa nchini wanakabiliwa na changamoto kutokana na uuzawaji wa mahindi kutokana na serikali kupiga marufuku uvushwaji wa mahindi nje ya nchi hali ambayo imesababisha mahindi mengi kubakia kwenye maghala.
Alitolea mfano katika mji wa Kibaigwa ambao una mahindi tani 10,000 yakiwa kwenye maghala ambapo wakulima wameshindwa kuyapatia soko la uhakika kutokana na serikali kuzuia uvushwaji wa mahindi nje ya nchi.
0 Comments