6/recent/ticker-posts

Wanachama Elimu Saccos Watakiwa Kuwa Wabunifu

Na Salum Vuai, Maelezo

WANACHAMA wa Ushirika wa Akiba na Mikopo Elimu (Elimu Saccos), wameshauriwa kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi ya pamoja miongoni mwao, il kujiandalia mazingira mazuri ya maisha ya baadae.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Wajasiriamali katia Benki ya CRDB Sebastian A.P. Masaki, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa mwaka wa ushirika huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ufundi Karume, Mbweni mwishoni mwa wiki.


Masaki alisema, katika kutimiza jambo hilo, ni vyema wajasiriamali, mbali ya kuwa wanachama wa ushirika, lakini waangalie uwezekano wa kuanzisha miradi ya pamoja kwa vikundi vidogo ili kujiongezea tija.

Alisema, kwa mfano watu watatu au wanne, wanaweza kuunganisha nguvu na kununua kitu kitakachowaingizia fedha kama vile basi la abiria, hata kama itabidi wakope, na baadae kusimamia vizuri uendeshaji wake.

Kwa kuwa kiwango cha mishahara wanachopata wakiwa kazini hakikidhi haja, aliwashauri kuanza kubuni miradi ya pamoja sasa kabla kusubiri kustaafu, ambapo alisema wakati huyo maisha yatakuwa magumu zaidi.

"Chukulia mfano, hivi sasa umeajiriwa lakini mshahara hautoshi, utakapostaafu utategemea pensheni ambayo ni asilimia 20 ya mshahara ulikuwa ukipata, bila kubuni namna ya kujiendeleza, utawezaje kuishi", alfahamisha.

Aidha, alishauri wanachama hao waanze kufikiria kubuni miradi mikubwa badala ya kutosheka kuwa wajasiriamali wadogo, ili wajihakikishie ustawi wa maisha yao na familia zao.

Alisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kuanzisha vitega uchumi, na kueleza kuwa katika zama hizi za ushindani wa kisoko, watu hawawezi kushindana kibinafsi bali lazima wawe wamoja kwa kuanzisha miradi mikubwa na yenye mwelekeo wa kuwakomboa kiuchumi.

Kwa upande mwengine, aliwataka wanaushirika hao kuzitumia kikamilifu rasilimali zilizopo nchini kama vile ardhi, bahari na maeneo mengine yanayoweza kuwa chachu ya kuwakomboa kutokana na umasikini.

"Umasikini tunautaka wenyewe kwani nchi yetu ina rasilimali nyingi lakini hatuzitumii, hizi ni zetu sio za kundi fulani lazima tuzichangamkie kwa kufuata taratibu na sheria za nchi", alisisitiza.

Alikosoa mtindo wa watu kuanzisha biashara za aina moja katika sehemu hiyohiyo, hasa kwa wengine kushindwa kuwa wabunifu mpaka wawaone wenzao wanauza bidhaa, na wao wanakwenda kujipachika hapo hapo.

Katika mkutano huo, wanachama wa ushirika huyo walisomewa ripoti mbalimbali za fedha na nyenginezo zihusuzo maendeleo ya Saccos hiyo.

Ushirika wa Akiba na Mikopo Elimu, ulianzishwa 1997 kwa lengo la kuwainua wanachama wake kimaisha, ukiwa na wanachama 61 na hadi mwezi Disemba mwaka jana ulikuwa na wanachama 2245.

Post a Comment

0 Comments