Na Othman Khamis, DODOMA
SERIKALI itaendelea kutoa taaluma kwa wananchi ili waepukane na tabia ya kujenga makaazi ya kudumu kwenye maeneo hatarishi ambayo huteta athari zinazopelekea kutokea maafa.
Waziri mkuu Mizengo Pinda alitoa kauli hiyo huko nyumbani kwake Dodoma, baada ya kupokea mchango kwa ajili ya wananchi walioathirika na mafuriko ya mvua iliyoukumba mkoa wa Dar es Salaam miezi michache iliyopita.
Mchango huo wa shilingi milioni 50,000,000, umetolewa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwasilishwa kwa waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Pinda alisema baadhi ya watu kwa kukosa taaluma ya kutosha wamekuwa na tabia ya kujenga maeneo ya hatari ambayo hayafai kwa makazi ya watu na matokeo yake ni hasara wakati inapotokea mafuriko.
Pinda alifahamisha kuwa kufuatia maafa yaliyowakumba wananchi wa Jangwani jijini Dar es salaam, serikali imetenga eneo la Mabwepande Bunju Mkoani Dar es Salaam ambapo wananchi wa Kata 300 wameshapatiwa viwanja na wengine wa kata 250 wanaendelea kushughulikiwa.
“Mwanzo ilikuwa kazi kuhamisha mtu kwenda eneo hilo, lakini wale waliobahatika kufika na kuona eneo lenyewe kwa vile tayari miundombinu imeshawekwa walifurahia eneo hilo”, alisema Pinda.
Alisisitiza kwamba serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi hao katika harakati zao za kuhamisha vifaa vilivyokuwepo katika makazi yao ya zamani.
Aidha alieleza kuwa serikali inaendelea kukabiliwa na changamoto ya kuomba misaada kwa ajili ya kuwasaidia wananchi walioathirika na mafuriko hayo wakiwemo pia wale waliokuwa wamepanga nyumba katika eneo hilo la mafuriko.
Pinda aliwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kuunga mkono harakati za kusaidia ndugu zao waliopatwa na janga hilo, huku akisema itakuwa ni faraja.
Mapema akikabidhi mchango huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, alisema mafuriko hayo yameathiri watu kadhaa na matokeo yake wengi kati yao wamekosa makaazi.
Balozi Seif alisema wananchi wa Zanzibar wamepokea kwa mshituko taarifa za janga na wameungana nao katika kuwapa pole katika kipindi kizito hasa kwa wale waliopoteza ndugu na jamaa zao.
Maafa yaliyoukumba Mkoa wa Dar es salaa na vitongoji vyake yalisababisha vifo vya watu 40, nyumba kadhaa kuzama na nyengine kubomoka na baadhia miundombinu kama vile barabara na nguzo za simu kuharibika kabisa.

0 Comments