SERIKALI inakusudia kubinafsisha huduma za kufanya usafi wa mji, kwa kuruhusu kazi hiyo kufanywa na kampuni za watu binafsi zitakazopenda kuendesha kazi hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ikiwa ni utaratibu wa mawaziri kuelezea majukumu yao ya utekelezaji.
Mwinyihaji alisema, wizara yake katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka, imeweza kufanya mambo mbali mbali ikiwemo suala la kuandaa mpango wa kubinafsisha huduma za usafi wa mji kwa kuruhusu kampuni binafsi kufanya hivyo.
Waziri huyo alisema wizara imeamua kuchukua uamuzi huo ikiamini kuwa lengo kuufanya mji wa Zanzibar kuwa katika hali ya usafi kwa wakati wote.
Alisema imelazimika kuzikaribisha kampuni binafsi kwani hivi sasa katika miji mbali mbali duniani kazi hiyo inafanywa na kampuni binafsi na sio serikali.
Dk. Mwinyihaji alisema umefika wakati serikali haiwezi kuendelea na mfumo wa sasa uliopo wa kusafisha mji na tayari imeshaanza kuutangaza mpango huo kwa wananchi ili kuwapa nafasi kwa wanaoweza kuomba kuifanya kazi hiyo.
Alifahamisha kuwa serikali itashirikiana na kampuni zitakazojitokeza na kupata nafasi ya kufanya kazi hiyo, ili lengo la mji wa Zanzibar kuwa safi liweze kufikiwa.
Alisema wizara hiyo inajiandaa kuweka kanuni ambazo zitaweza kuwapa adhabu watu wataobainika kutupa taka ovyo na kuwataka wananchi kupenda tabia ya usafi.
Aidha alisema mipango inaandaliwa kutafuta majiko ya kuchomea taka ikiwa ni hatua itayopunguza gharama za utupaji wa takataka kwa kuzingatia kuwa zaidi ya asilimia 86 ya taka hizo ni mboji.
Alisema uwezo uliopo hivi sasa katika majaa ya Zanzibar ni kubeba asilimia 45 huku kukiwa na mahitaji ya asilimia 70 ya taka zinazotakiwa kutumia majaa ambapo mradi huo utajenga majaa mapya 193.
Akizungumzia urandaji wa wanyama mjini, Dk. Mwinyihaji alisema wanakusudia kuanzisha msako mkali wa kukamata wanyama wanaoranda ovyo, baada ya kuandaa kamati maalum ya wilaya ambayo itaweza kutumia busara katika kudhibiti tatizo hilo ikiwa ni hatua ya kuondoa kuwapo malumbano wakati wa utekelezaji wa oporesheni hiyo.
Alisema mpango huo utaenda sambamba na uimarishaji wa usafi katika mitaro baada ya serikali kupata mradi mkubwa wa kuimarisha huduma za miji Zanzibar (ZUSP), ambao utajumuisha ujenzi wa michirizi ya maji ya mvua na kufanya ukarabati wa ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua katika maeneo ya ng’ambo.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa na serikali mwisho wa mwaka huu kwa vile tayari zabuni za kufanya kazi hiyo zimeanza kutangazwa pamoja na kufanyika kwa tathmini za mwisho ikiwa ni hatua itayoweza kupunguza athari za kimazingira.
Waziri huyo, alisema wakati wakisubiri mradi huo kuanza wanakusudia kuizibua mitaro ya maji machafu ndani ya kipindi cha miezi mitatu ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mvua za masika.
Akifafanua zaidi juu ya mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Mzee Khamis Juma, alisema mradi huo unatarajia kutumia dola za kimarekani zaidi ya milioni 7 ambapo utahusisha ujengaji wa majaa mapya.
Kuhusu suala la hali ya Vyuo vya Mafunzo, alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na msongomano katika magereza ikiwa pamoja kuimarisha kiutendaji.
Alisema katika kulitekeleza hilo serikali inakusudia kukaa pamoja na Idara ya Mahakama kuona vipi wataweza kuharakisha uendeshaji wa kesi.
Aidha, Waziri huyo alisema Wizara hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwa pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma katika halmashauri ambapo kuanzia sasa itaweka wataalamu ambao watakuwa wakifanya kazi zao kisekta.
Waziri huyo alisema katika kuona Wizara hiyo inaimarisha huduma zake inakusudia kuanza ujenzi kwa ajili ya ofisi za wizara hiyo itayojengwa Mazizini Mjini Uguja.
0 Comments