MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema jambo linalowagusa zaidi Wazanzibari katika kuelekea kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ni kuwa na mfumo wa Muungano ambao hauwabani katika nyanja zote ikiwemo kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Alisema, Wazanzibari ambao tayari wanayo katiba yao iliyo sawa na ile ya Jamhuri ya Muungano, suala kubwa wanalopaswa kulizingatia ni kuwepo katiba mpya itakayotoa haki sawa kati ya pande mbili za Muungano huo, bila ya kuwepo dhana ya ukubwa au udogo.
Maalim Seif aliyasema hayo jana hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar, alipokuwa akifungua mkutano wa pili wa hali ya siasa Zanzibar, ulioandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Wazanzibari watakuwa na fursa ya kipekee kuamua aina gani ya Muungano wenye maslahi kwao, uwe kama ulivyo sasa, uwe Muungano wa serikali tatu au Muungano wa mkataba kwa mambo watakayokubaliana pande mbili, badala ya ule wa kufungana kikatiba”, alisema Maalim Seif.
Alisema jambo la muhimu katika kufanikisha lengo hilo, ni wananchi wote wa Zanzibar wanapaswa wajipange vizuri, ili wakati wa kutoa maoni utakapofika waweze kutoa maoni yenye maslahi kwao.
Alieleza kwamba, yeye pamoja na viongozi wengine kama vile Rais Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na viongozi wengine wamekuwa wakiwahimiza wananchi wa Zanzibar kufuatilia kwa makini mchakato wa kupata katiba hiyo mpya, itakayokuwa na maslahi kwa wananchi wa Zanzibar na wenzao wa Tanzania Bara.
Maalim Seif alisema malengo hayo yatakapoweza kufikiwa migogoro, malalamiko na manung’uniko mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza tokea Muungano huo ulipoasisiwa mwaka 1964, yataweza kupungua na kuondoka kabisa.
Akizungumzia serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif alisema mfumo huo wa serikali umeleta faida kubwa kwa Zanzibar, kwani umeweza kuondoa kabisa tabia ya mivutano inayotokana na itikadi za kisiasa.
Alisema huko nyuma kabla ya kufikiwa maridhiano wananchi wa Zanzibar walikabiliwa na mifarakano ya hali ya juu, hali iliyosababisha kwa kiasi kikubwa maendeleo yao kusuasua.
Alieleza kuwa kupatikana kwa maridhiano ya kweli na baadaye kuundwa serikali ya aina hiyo, kumelata umoja miongoni mwa wananchi na hivi sasa Wazanzibari wote wanachangia na kushiriki katika harakati za maendeleo ya nchi yao.
Alisema miongoni mwa wananchi hao ni wale ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi nje ya Zanzibar, ambao hivi sasa wamekuwa na hamu kubwa ya kuona Zanzibar inapiga hatua kubwa ya maendeleo.
Alifahamisha kuwa faida nyengine zinazopatikana hivi sasa ni kuonesha mshikamano wa wanajamii wote, kama hali iliyojitokeza mwezi Septemba mwaka jana, baada ya kutokea maafa ya kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islander, jambo ambalo huko nyuma wakati kukiwa hakuna maelewano, mshikamano kama huo usingeweza kupatikana.
Alisema mbali na wananchi wenyewe wa Zanzibar, pia wawekezaji vitega uchumi kutoka nje ya nchi wameridhishwa na hali ya amani na utulivu, ambayo ni muhimu katika shughuli za kufungua miradi ya kiuchumi.
Akizungumzia changamoto zinazojitokeza kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif alisema kati ya hizo ni kuwepo baadhi ya viongozi na watu ambao hawafurahishwi na maridhiano ya Wazanzibari.
“Watu hao ni wachache,baadhi yao wamekuwa wakijaribu kutia fitna, ili kuvuruga maelewano, kwa bahati mbaya yapo magazeti machache yanayotolewa Tanzania bara ambayo yamepania kuleta chokochoko, ili kuvuruga kuaminiana kulikojengeka”, alionya Maalim Seif.
Hata hivyo, Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, alisema azma ya watu hao wachache haitafanikiwa na badala yake mshikamano na umoja miongoni mwa Wazanzibari utaendelea kuimarika.
Alisema kwamba watu hao wenye mawazo tenganishi watashindwa, kwa sababu wananchi wengi wa Zanzibar wanaona hali ya umoja na maelewano miongoni mwao ina faida kubwa zaidi kuliko kutengana.
0 Comments