6/recent/ticker-posts

Walimu Wataobainika Kuwapa Mitihani Wanafunzi Kukiona

Na Khamisuu Abdallah

NAIBU waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad amesema wizara itawashughulikia walimu watakaobainika kuwa iliwasaidia wanafunzi kuipata mitihani ya kidato cha nne kwa njia ya udanganyifu.

Naibu huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza Wawakilishi uliopo Kikwajuni mjini hapa alipokuwa akizungumza kwenye kongamano lililowashirikisha walimu wakuu wa skuli za Unguja.

Alisema ikibainika wapo walimu kwa njia moja ama nyengine walishiriki kuwapatia mitihani kwa njia ya udanyanyifu wanafunzi wa kidato cha nne, wizara itawawajibisha walimu hao.


Kauli ya Naibu huyo imekuja ambapo mamia ya wanafunzi kutoka skuli 30 za Zanzibar waliofanya mitihani ya kidatu cha IV mwaka jana kufutiwa matokeo yao huku sababu bayana ikiwa haijaelezwa.

Naibu huyo alisema taifa linapata hasara kubwa pindipo wanafunzi wataachiliwa kufanya mitihani kwa udanganyifu, hivyo lazima tabia hiyo ikomeshwe.

Alisema tabia ya walimu kuwapa mitihani ya udanganyifu wanafunzi huondosha sifa ya vipaji kwa wanafunzi wao, na kulifanya taifa kukosa sifa ya vijana wasomi hali itakayokwamisha maendeleo.

"Kama mwalimu anahisi uwezo wake mdogo aachie ngazi kwa kukaa pembeni, nia ya wizara ni kuwapa elimu bora wanafunzi kwa ajili ya maisha yao",alisema Naibu huyo.

Aliwataka walimu wanaopewa jukumu la kusimamia mitihani kuwa waangalifu ili wasiwatumbukize wanafunzi kwenye mambo ya udanyanyifu.

Aidha Zahra alisema wapo baadhi ya walimu wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kutoingia madarasani kama inavyotakiwa na hata walimu hao wakiingia hawasomeshi kikamilifu.

Alikitaka chama cha Zanzibar (ZATU), kuwahimiza walimu ambao ndio wanachama wake kufanyakazi kwa bidii na kufuata miiko ya kazi yao sambamba na uwajibikaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (ZATU), Rabia Nassor Majid alisema umefika wakati walimu kuacha kuwekea chuki wanapokuwa kazini na badala yake washirikiane pamoja.

Alifahamisha kuwa kutopendana baina yao na kuwekeana chuki kunakwamisha maendeleo ya elimu, huku akihimiza mshikamano na mashirikiano baina yao.

Kongamano hilo la siku moja ni sehemu ya shamra shamra za kutimiza miaka 10 tangu kuzanzishwa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU).

Post a Comment

0 Comments