Na Madina Issa
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, imesema licha ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza, imejipanga kuimarisha huduma za afya katika hospitali na vituo vyake vyote vya afya nchini.
Waziri wa Afya Juma Duni Haji, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wizara yake imedhamiria kutatua kero zilizomo katika vitengo vya wizara hiyo, ikiwemo uhaba wa madaktari, wauguzi na dawa katika hospitali zake Unguja na Pemba.
Alisema, miongoni mwa jitihada za serikali, ni pamoja na kupiga vita maradhi mbalimbali ya kuambukiza, kwa watoto, ikinamama na jamii kwa jumla.
Alifahamisha kuwa, huduma za chanjo za mama na watoto, lishe, pamoja na mapambano dhdi ya ugonjwa wa malaria, zimeimarishwa kwa kiasi kikubwa na kuifanya Zanzibar kuwa nchi ya kupigwa mfano kwa mafanikio iliyopata katika kupunguza ugonjwa huo ambapo sasa upo chini ya asilimia moja.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa elimu ya afya ni muhimu kwa jamii na ndio msingi wa kinga, na kwamba endapo wananchi hawataelimishwa na kufahamu, mafanikio ya kushinda vita dhidi ya maradhi thakili hayataweza kupatikana.
Katika mpango wa kuendelea na kupambana na malaria, Duni alisema serikali inakusudia kusambaza vyandarua vipya vilivyotiwa dawa kuanzia mwezi huu na kuendelea katika kipindi cha miezi sita katika shehia zote za Unguja na Pemba.
Alisema jumla ya vyandarua 700,000 vilivyotolewa msaada na mashirika mbalimali ya misaada ya kimataifa, vitagaiwa nchi nzima na wizara itahakikisha kuwa kila familia itapata chandarua, baada ya zoezi la kujiandkisha litakalofanywa kwa ushirikiano na masheha.
Kwa upande mwengine, alikiri kuwa wizara yake inakabilwia na uhaba wa madaktari na wauguzi, lakini jitihada zinafanywa kuajiri wafanyakazi wapya watakaosaidia kupunguza uhaba huo.
Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, jumla ya madaktari 30 hadi 38, wanatarajiwa kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo yao.
Alitaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Kwa upande wa maslahi ya wafanyakazi hasa madaktari, Waziri huyo alisema serikali imeamua kupitia upya maslahi ya madaktari ili kuyaimarisha na kuondoa malalamiko ya mara kwa mara.
Alisema zoezi hilo tayari limeanza kufanywa kwa ushirikiano na Wizara ya Nchi (OR) Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na kwamba stahiki zao zitaanza kulipwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Alisema hatua hiyo inalenga kuondoa malakamiko yasiyo ya lazima, na kuiepusha nchi na migomo kama iliyotokea Tanzania Bara.
0 Comments