6/recent/ticker-posts

58 m/- Kusomesha Mayatima wa M.v Spice

Na Salum Vuai, Maelezo

KAMATI ya Saidia Zanzibar, jana ilikabidhi hundi ya shilingi 58,000,000 kwa jumuiya inayotoa huduma kwa jamii 'Zanzibar Outreach Programme' (ZOP), kwa ajili ya kusaidia kuwasomesha watoto waliopoteza wazazi wao katika ajali ya kuzama kwa meli ya M.v Spice Islanders mwezi Septemba mwaka jana.

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika hoteli ya Serena Inn iliyopo Shangani mjini Zanzibar, ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Zanzibar Bobby Mackena, alisema kutokana na msiba huo mkubwa wa taifa, jumuiya yake iliamua kuwaendea watu na taasisi mbalimbali ili kuziomba msaada kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa ajali ya M.v Spice.

Alieleza kuwa baada ya watu kuhamasika, michango mingi imekuwa ikipokelewa kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo fedha, nguo, vitu vya kuchezea watoto, dawa na vyenginevyo, hali iliyosaidia kuwafaraji watu waliokumbwa na kadhia hiyo.


Alifahamisha kuwa, kamati yake ilifanya utafiti wa kina ili kutambua ni jumuiya gani inayoweza kufanya nayo kazi ya kusambaza misaada hiyo kwa walengwa, na kuvutiwa na utendaji wa ZOP, ambayo imesajiliwa kama asasi ya kiraia na tayari ina uzoefu wa kutosha wa kuwafikia watu wanaoishi katika mazingira magumu.

Alichukua fursa hiyo kuzishukuru taasisi zote zilizoonesha ushirikiano pamoja na watu binafsi waliosadia kwa njia tafauti, kufanya kazi ya uokozi na uopoaji watu kwenye tukio la kuzama kwa meli hiyo ambapo watu 203 walipoteza maisha na wengine 1,370 kupotea baharini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Saidia Zanzibar Simai Mohammed Said, alisema jitihada za kutafuta misaada zaidi zitaendelea, na kuwahakikishia wananchi na serikali kuwa, hakuna hata senti moja itakayotumika kinyume na malengo ya kamati yake.

Katibu wa ZOP Dk. Noufal Kassim Mohammed, alisema zoezi la kuwatafuta watoto waliopoteza wazazi wao katika ajali hiyo lilifanyika kwa makini na kushirikisha watu tafauti katika shehiya husika, ambapo pia imebainika kuwa wengine wanaishi Tanzania Bara walikochukuliwa na jamaa zao.

Alisema kimsingi, lengo lao ni kuwasaidia kielimu watoto waliofiwa na baba zao ambao kwa kawaida ndio wanaotegemewa na familia, au waliopoteza wazazi wote wawili, lakini ikaonekana wapo waliokuwa wakishughulikiwa na mama zao wajane ambao nao walifariki katika mkasa huo, hivyo nao watanufaika na msaada huo.

Alieleza kuwa lengo ni kuwasomesha watoto wenye umri wa kuanzia miaka 7 hadi 18, ambao tathmini inaonesha wanafikia vigezo hivyo.

Dk. Noufal alifahamisha kuwa wakati wa zoezi la kutafuta taarifa za watoto hao kwa kutumia vituo mbalimbali vilivyowekwa kujiandikisha Unguja na Pemba, jumla ya watoto 153 wameonekana wanastahiki msaada huo, ambapo mlezi wa kila mtoto atapewa kati ya shilingi 45,000 na 60,000 kila mwezi, nusu yake zililenga mahitaji ya skuli na nyengine kwa huduma za nyumbani.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Zanzibar Abdulsamad Said, ameiomba serikali, pamoja na kazi yake nzuri, kufanya kazi kwa karibu na ZOP katika kuhakikisha walenga wa misaada iliyotolewa na taasisi na watu mbalimbali kuwafariji waathirika wa ajali ya M.V. Spice wanafikiwa na kunufaika kikamilifu.

Post a Comment

0 Comments