6/recent/ticker-posts

Dk. Ndalichako: Waliofutiwa Matokeo Wamechakachua Mitihani

 Abainisha vielelezo kadhaa vilivyokamatwa
Awanyooshea vidole walimu, wasimamizi kuhusika
Asema Baraza lake halikumuonea mtu

Na Mwantanga Ame

BARAZA la mitihani Tanzania (NECTA), limesema wanafunzi wa Zanzibar waliofutiwa matokeo yao ya mtihani wa kidato cha nne walifanya udanganyifu, huku baadhi yao wakishirikiana na wasimamizi wa mitihani.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Lazaro Ndalichako, aliyasema hayo jana ukumbi wa hoteli ya Bwawani, mjini hapo alipokuwa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya sakata la mamia ya wanafunzi kufutiwa matokeo ya mtihani ya kidato cha nne.

Alisema baadhi ya walimu na wasimamizi wa mitihani hiyo wamehusika kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa mitihani hiyo baada ya kubainika kwa vielelezo kadhaa vinavyothibitisha kufanyika kwa udanganyifu huo.


Dk. Ndalichako alisema hakuna aliyeonewa na wala Baraza halina nia ya kumuonea mtu juu ya kufutwa kwa matokeo hayo, bali imethibitika kuwa wanafunzi hao walichakachua baada ya kukutwa na meseji kwenye simu zao zikiwa na majibu ya mitihani.

Aidha katika baadhi ya vielelezo wasimamizi walikamata vikaratasi walivyokuwa wanafunzi hao wakipasiana katika kupeana majibu ya mitihani hiyo, huku pia ukiwepo mfanano usio wa kawaida katika majibu.

Katibu huyo alifahamisha baadhi ya walimu ikiwemo mmoja kutoka skuli ya Kiboje anahusishwa na sakata hilo baada ya kuliandikia Baraza la Mtihani barua inayotoa malezo yanayomhusisha mtahiniwa wa masomo ya faragha na mwanafunzi wa skuli.

Alisema mazingira ya maelezo ya barua hiyo yameonesha baadhi ya wasimamizi na walimu hao walihusika katika sakata hilo baada ya kukiri kuwepo kwa utata wa karatasi za mtihani wa mmoja ambayo ilikutwa ndani ya nyumba ya mwalimu miezi mitatu baada ya kumalizika kwa mitihani.

Akifafanua zaidi alisema utata huo unakuja baada ya kubaini karatasi halisi alizojaza mwanafunzi huyo hazikuwemo katika bahasha za makusanyo ya mitihani iliyofanyika, huku kukiwa na mtihani uliofanyika uliotumia namba zake kwa mwanafunzi wa faragha.

Alisema jambo la kushangaza namba ya mwanafunzi huyo pia ilikutwa katika bahasha la wanafunzi wa kawaida, lakini ikiwa ina majibu ya mtihani wa wanafunzi wa faragha.

Kutokana na sakata hilo, Dk.Ndalichako, alisema wanaamini kuwepo kwa mazingira yanaoonesha baadhi ya walimu na wasimamizi kuhusika kutokea matokeo hayo.

Alisema wizara husika tayari imeanza kuwafanyia uchunguzi baadhi ya walimu na wasimamizi wa mitihani hiyo kutokana na kubaini baadhi yao kutowajibika ipasavyo.

Alisema mtihani uliomalizika baadhi ya wanafunzi wa Zanzibar kufanya vibaya kulikosababishwa na udanganyifu baada ya mamlaka ya uchunguzi wa maandiko iliyochini ya wizara ya Elimu kubaini kulikuwa na maandiko yanayofanana.

Kutokana na hali hiyo Dk.Ndalichako, alisema kwa mujibu wa kanuni ya 6 kifungu cha 2 (b), kinaelezea kuwa mwanafunzi anaekiuka taratibu za mitihani anaweza kufutiwa mtihani na hatua waliyoichukua kuwafutia matokeo ipo kihalali.

Akizungumzia juu ya ukubwa wa adhabu waliyotoa kutaka kurudia mtihani huo baada ya miaka mitatu, Baraza hilo imelifanya kwa huruma lakini bado watakaa kuona kama wanastahili kuipunguza.

Alisema wanalazimika kuona adhabu hiyo inabakia kutokana na kuwaandaa wanafunzi kutokubaliana na vitendo vya kufanya udanganyifu katika mitihani yao kwani ikiwa watapewa adhabu fupi wataweza kurudia mchezo huo.

Hata hivyo Katibu huyo, aliwataka wazazi, walimu na wanafunzi kuacha tabia ya kushabikia vitendo hivyo kwa vile vinawapa wakati mgumu watoto wao baada ya kumaliza masomo kuonekana ujuzi wao ni mdogo ikilinganishwa na elimu aliyokuwa nayo.

Katibu huyo alisema wanaotarajiwa kuchukuliwa hatua baada ya uchungzi wao kufanyika bado hawajajua idadi ya walimu wataohusika na kashfa hiyo.

Mamia ya wanafunzi katika skuli 30 za Zanzibar wamefutiwa matokeo yao ya kidato cha nne yaliyofanyika mwaka jana.

Post a Comment

0 Comments