Na Asya Hassan
IKIENDELEA kupigana ili kujinusuru na hatari ya kushuka daraja, timu ya Mundu, juzi iliiweza kuwafyeka maafande wa Polisi kwa kipigo cha bao 1-0, kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka Zanzibar inayoelekea mfundani.
Mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa Amaan, ulikuwa wa ushindani mkubwa, huku kila timu ikijaribu kusaka ushindi ili kujihakikishia inavuka salama na kubaki katika ligi hiyo msimu ujao.
Hata hivyo, hadi zinakwenda mapumziko, hakuna nyavu iliyokuwa imehujumiwa.
Mundu ilifanikiwa kupata bao lake pekee katika dakika ya 72, ambalo liliwekwa nyavuni na Ibrahim Masanyiwa.
Na katika mchezo ulipigwa uwanja wa Mao Dzedong siku hiyo, timu ya Zimamoto ikaizima Chipukizi kwa kuichapa mabao 3-1.
Mabao ya Zimamoto yalifungwa na mchezaji Ramadhan Abdallah, Hakim Khamis pamoja na Hamad Mgeni, huku Fakih Mwalimu akiifungia Chipukizi bao la kujifariji.
0 Comments