6/recent/ticker-posts

Barabara ya Konde-Msuka kuinua kipato cha wananchi

Na Masanja Mabula,Pemba
HALI za kimaisha kwa wananchi wa Shehia ya Msuka Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba huenda zikaimarika wakati a ujenzi wa barabara ya Konde - Msuka utakapokamilika.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini kwao wananchi hao wamesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo ambayo inaendelea kujengwa kwa kiwango cha kifusi itakuwa ni mkombozi kwao kwani wataweza kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa wakati.

Walisema licha ya barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha kifusi lakini kwa hatua iliyofikiwa kwa sasa inatia matumaini kwani shida na usumbufu waliokuwa wakiupata hapo awali umepungua.

Hamad Khamis Mohammed (48) na Shaame Juma Omar (50) wote kwa pamoja wameipongeza kamati ya maendeleo ya Jimbo la Konde kwa kuamua kutafuta wafadhili wa kujenga barabara hiyo.

Kwa upande wake Mhandisi wa ujenzi wa barabara hiyo, Juma Zubeir alisema hatua ya kwanza ya ukarabati wa barabara hiyo uko mbioni kukamilika ambapo hatua ya pili itafuata baadae.

Alifahamisha hatua ya tatu ni kumwaga kifusi ambapo kwa hatua zote hizo jumla ya shilingi milioni 300 zitatumika ambazo zimepatikana kama msaada kutoka serikali ya Japan .

Hata hivyo, Katibu wa Kamati ya Maendeleo jimbo la Konde, Ismail Juma aliwataka wananchi wa Msuka kuupokea mradi huo na kuutunza kwani umelenga kuwaondoshea shida walizokuwa wakizipata hasa wakati wa mvua.

Kukamilika kwa mradi wa barabara hiyo pia kutapelekea kuimarika kwa bandari ya Msuka ambayo inatumiwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za kisiwa cha Pemba kwani ndio bandari kubwa inayotumiwa na wachuuzi wa samaki.


Post a Comment

0 Comments