Na Husna Mohammed
BARAZA la Habari Tanzania (MCT) ofisi ya Zanzibar,
limesema licha ya kuwepo baadhi ya vyombo vya habari vinavyokwenda kinyume na
maadili na kuchochea ghasia lakini tasnia ya habari Zanzibar imekua.
Meneja wa baraza hilo ofisi za
Zanzibar, Suleiman Seif Omar, aliuambia ujumbe wa maofisa wa balozi wa baadhi
ya nchi za Ulaya waliotembelea ofisi za baraza hilo Mlandege mjini hapa.
Maofisa hao walitaka kujua wajibu
wa vyombo vya habari Zanzibar
hasa katika kutekeleza wajibu wao wa kutoa taarifa kwa umma.
Meneja huyo, alisema vipo baadhi ya
vyombo vya habari hasa vinavyofanyia kazi Tanzania Bara vimekuwa vikipotosha
wananchi hasa kwa habari zinazohusiana na uchochezi na vurugu ambazo wamekuwa
wakizipa nafasi kubwa kinyume na hali inavyokuwa pamoja na kuzitia chumvi.
“Tumekuwa mstari wa mbele
kuelimisha vyombo vya habari kupitia baraza la habari Tanzania ili kutekeleza
majukumu yao bila ya kukiuka maadili ila ni vyombo vichache vinavyofanya hivyo
jambo ambalo wakati mwengine linachangiwa na wahariri,” alisema.
Aidha Meneja huyo alisema vyombo
vya habari Zanzibar, vimekuwa vikisaidia kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa
kulinda amani na utulivu.
Sambamba na hilo,aliuambia ujumbe
huo kuwa Baraza la Habari Tanzania
limekuwa na msimamo wa pamoja juu ya kuingizwa vyombo vya habari katika katiba
mpya kuwa ni muhimili wa nne kutokana na umuhimu wake katika nchi.
Nae Jussi Nummelin, ofisa Ubalozi
wa Finland, alilitaka baraza la Habari kuendelea kutekeleza wajibu wake wa
kuelimisha wananchi juu ya kulinda amani na utulivu.
Aidha alisema vyombo vya habari
vinapaswa kusimamiwa na MCT kwa kuhakikisha havivunji maadili ya habari
sambamba na kuhimiza amani ya nchi na wananchi kwa ujumla.
Ujumbe huo wa mabalozi unatoka nchi
za Norway, Finland, Uholanzi na Jumuiya ya nchi za Ulaya.
0 Comments