6/recent/ticker-posts

Jamii Yahimizwa Kuwatembelea Wazee.

Na Masanja Mabula,Pemba
JAMII imetakiwa kuwa na utaratibu wa kuwatembelea na kuwafariji wazee, hasa wale wanaoishi katika nyumba za kulelea wazee zilizotengwa na serikali.

Mkuu wa wilaya ya Wete, Omar Khamis Othman, alisema hayo wakati akizungumza na wazee katika maadhimisho ya siku ya wazee Duniani ambayo kwa Pemba yaliadhimishwa katika nyumba za kulelea wazee Limbani Wete.

Alisema pamoja na serikali kuwaandalia mazingira mazuri wazee, lakini jamii nayo inatakiwa kutambua wajibu wake katika kuwatembelea ili kuwapa matumaini ya kuwepo katika nyumba hizo.

Aidha alisema serikali inatambua mchango uliotolewa na wazee katika kuleta ustawi na maendeleo ya nchi na kwamba itaendelea kuwaenzi na kuwatunza kwa kuwapatia mazingira bora.

"Pamoja na serikali kuwaandalia mazingira mazuri ya makaazi wazee, lakini jamii nayo inatakiwa kuwa na kawaida ya kuwatembelea na kuwafariji kwa kuwatatulia baadhi ya changamoto zinazowakabili,” alisema.

Taarifa ya Idara ya Ustawi iliyosmwa na Afisa Ustawi Pemba, Mohaamed Ali Hamad alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee ikiwa na pamoja na kutokuwa na malipo ya pensheni kwa waazee.

Alisema tofauti ya malipo kwa wazee ni moja na mambo yanayohitaji kujadiliwa na serikali ili kuwepo na uwiano wa malipo yanayotolewa na serikali.

"Posho la mkononi kwa wazee wanaoishi kwenye nyumba za kulelea ni shilingi 40,000na posho la shilingi 5000 kwa wazee wanaaioshi vijijini halitoi haki sawa kwa wazee kwani hata mahitaji yao yanalingana, hivyo kunahitaajika marekebisho ili kuwepo na uwiano,” alisema.

Wakisoma risala yao wazee hao wameiomba serikali kuendelea kuthamini mchango wao katika kuleta maendeleo ya nchi, hivyo ni vyema serikali kuangalia uwezekano wa kuwandalia sheria na sera maalumu zitakazo walinda dhidi ya vitendo viovu.

Post a Comment

0 Comments