MAELEZO
YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA KATIKA
MKUTANO WA TANZANIA CENTER FOR DEMOCRACY, KUHUSU TAFAKURI NA MARIDHIANO
KUELEKEA KATIBA MPYA: WHITESANDS HOTEL,
DAR ES SALAAM, 12 FEBRUARI, 2014
___________________________________
1.0 UTANGULIZI
Katika nchi yoyote, msingi wa
uendeshaji wa nchi unategemea Katiba ambayo ni sheria kuu. Sheria zote hutungwa
kwa kuzingatia masharti ya Katiba. Katiba huainisha misingi ya Taifa, mgawanyo
wa madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, usimamizi wake, mgawanyo na
ukomo wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola. Kwa ujumla Katiba ni
makubaliano ya wananchi husika kuhusu utaratibu na kanuni za uendeshaji wa
mambo mbalimbali katika nchi yao .
Kutokana na maana hiyo ya
Katiba, utungaji wake unatakiwa kuwa shirikishi kwa maana ya kuwahusisha
wananchi katika hatua zote za mchakato wa kupata Katiba. Kadri mchakato wa
kuandika Katiba unavyowashirikisha wananchi kwa mapana, ndivyo kukubalika,
kuheshimika na utekelezaji wa Katiba utakavyokuwa rahisi. Wananchi
wanaposhiriki katika utungaji wa Katiba, na pale matakwa yao
yanapozingatiwa ndani ya Katiba, Wananchi hao huimiliki Katiba hiyo na kuiona
kuwa ni Katiba yao .
Wananchi huona hivyo kwa sababu licha ya kushiriki lakini pia katiba hiyo huakisi
utashi wao na ndoto zao na hivyo kukubali kuongozwa na masharti yaliyomo ndani
ya Katiba.
Mchakato wa katiba kwa kadri
unavyowashirikisha wananchi, ndivyo unavyowezesha kupatikana kwa mwafaka wa
kitaifa kuhusu misingi, malengo na namna serikali na vyombo vyake
vitakavyoongoza nchi. Mwafaka huo huzaa katiba ya wananchi ambayo inaimarisha
umoja, udugu, ushirikiano na mshikamano katika Taifa kwa maendeleo na ustawi wa
jamii.
1.1 Maana na sababu za Mchakato wa Katiba
Mchakato wa Katiba hulenga
kupata Katiba Mpya au kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo. Michakato mingi ya
Katiba hujumuisha Kanuni na hatua kama ifuatavyo:
(a) kukubaliana kuhusu mambo yote yanayohitajika na kupanga malengo;
(b) kukubaliana kuhusu vyombo vya Kusimamia na utaratibu utakaotumika;
(c) kuandaa Wananchi kwa kutoa elimu ya Katiba;
(d) kukusanya Maoni ya Wananchi wa aina zote;
(e) kushauriana na Wataalam;
(f) kujifunza kutokana na Uzoefu wa Nchi mbalimbali;
(g) kuchambua na kutathmini maoni ya Wananchi;
(h) kuandika Toleo la Kwanza la
Rasimu ya Katiba;
(i) Wananchi Kujadili Toleo la Kwanza
la Rasimu ya Katiba;
(j) Kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba;
(k) Bunge Maalum kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba;
(l) Wananchi kuridhia Katiba Iliyopendekezwa na Bunge Maalum
kupitia Kura ya Maoni;
(m) kuzindua kutumika kwa Katiba Mpya;
(n) utekelezaji wa Katiba Mpya.
Utekelezaji wa Masuala na
hatua zote zilioainishwa hapo juu ndio unatafsiriwa kuwa “Mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba.”
Katika mchakato wa Mabadiliko
ya Katiba unaoendelea katika nchi yetu, Kanuni na hatua hizi zimeainishwa
katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.
Msingi wa kuwa na mchakato wa
katiba ni kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki katika hatua zote za kupata
Katiba na hivyo kuijengea uhalali.
2.0 UTARATIBU WA KUFANYA MABADILIKO YA KATIBA
Katika mchakato wa mabadiliko
ya Katiba, zipo njia kadhaa ambazo hutumika. Njia hizo ni:
(a) Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba;
(b) kuunda Tume ya kuandaa
Katiba kupitia sheria zilizopo; au
(c) Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya katiba.
2.1 Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba
2.2 Kuunda Tume ya kuandaa
Katiba kupitia sheria zilizopo
Utaratibu mwingine wa
mchakato wa mabadiliko ya katiba hufanywa kupitia Tume inayoundwa kwa mujibu wa
sheria zilizopo ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali
katika Nchi. Chini ya utaratibu huu, Rais au Waziri mwenye dhamana ya masuala
ya katiba, kwa mamlaka anayopewa na sheria husika huunda Tume au Kamati za kushughulikia
mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Tume au Kamati inayoundwa
hupatiwa hadidu za rejea na muda maalum wa kukamilisha mchakato. Ripoti ambayo
itaandikwa kutokana na mchakato uliofanyika, hutumiwa na Serikali kuandaa
Rasimu ya Katiba au sheria ya marekebisho ya Katiba. Hata hivyo, licha ya
mchakato huu kutowashirikisha wananchi kwa upana na uwazi, Serikali hailazimiki
kufanya mabadiliko yoyote ya katiba na inaweza kukalia Ripoti na kupuuza
matakwa ya wananchi.
Aidha, mchakato wa mabadiliko
unaofanywa na Tume au Kamati kupitia utaratibu huu huzingatia hadidu za rejea
zilizotolewa na Serikali, ambazo wakati mwingine haziakisi, matakwa au madai ya
wananchi. Ghana , Uganda
Zimbabwe na Zambia
ni miongoni mwa nchi zilizowahi kufanya au kujaribu kufanya mabadiliko ya
Katiba kwa kutumia utaratibu huu.
2.3 Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya katiba
Utaratibu mwingine wa
mchakato wa mabadiliko ya katiba ni wa kutunga sheria mahsusi ya kushughulikia
mabadiliko ya katiba. Katika utaratibu huu, sheria inayotungwa hueleza
utaratibu wa mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Utaratibu huu ni shirikishi kwani wananchi
hushirikishwa kisheria katika hatua zote muhimu za uandikaji wa katiba yao . Chini ya utaratibu
huu, hadidu za rejea hutolewa na sheria yenyewe badala ya Rais au Waziri.
Aidha, Tume hupewa jukumu la kuratibu, kukusanya maoni ya wananchi, kuyachambua
na kutathmini maoni kabla ya kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba. Mara baada ya
kuandaa Rasimu ya Katiba, wananchi hupewa tena fursa ya kutoa maoni yao kabla ya Tume au
Kamati kuifanyia marekebisho na kuiwasilisha katika Baraza au Bunge Maalum la
Katiba.
Baraza au Bunge Maalum huwa
na jukumu la msingi la kuijadili na kuipitisha Rasimu ya Katiba. Katika baadhi
ya nchi kama vile Afrika Kusini , Ghana na Uganda , mchakato wa Katiba Mpya
ulikamilishwa na Bunge Maalum. Baadhi ya nchi pia hazikutumia Bunge Maalum na
badala yake, Rasimu ya Katiba ilipigiwa kura ya “Ndio” au “Hapana” baada ya
kutoka kwenye Tume au Kamati. Kwetu Tanzania , Sheria inayosimamia
mchakato wa mabadiliko ya Katiba imeainisha hatua zote tatu ambazo ni Tume
kuandaa Rasimu ya Katiba, Bunge Maalum kujadili Rasimu ya Katiba na kupitisha
Katiba ambayo itapendekezwa kwa wananchi ili kuipigia kura ya maoni.
3.0 MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA
Mwaka 2011, Taifa la Tanzania
lilianzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba. Kwa mara ya kwanza katika
historia ya Tanzania ,
Bunge lilitunga sheria mahsusi ya kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Sheria hiyo inayoitwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imeweka
masharti kuhusu usimamizi na uendeshaji wa mchakato wa mabadiliko ya katiba.
Sheria hii imempatia mamlaka Rais kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya
kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar .
Katika kutekeleza matakwa hayo,
Sheria ilimtaka Rais kualika Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu, Jumuiya
za Kidini, Asasi za Kiraia, Jumuiya na Taasisi zisizo za Kiserikali na Makundi
ya Watu wenye Malengo Yanayofanana kupendekeza majina ya watu wanaoweza
kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume .
Sheria hiyo imeainisha
utaratibu wa utendaji kazi wa Tume na
Hadidu za Rejea ambazo ni:
(a) kuratibu na kukusanya maoni ya Wananchi;
(b) kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba
yanayohusu mamlaka ya wananchi, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa
sheria na utawala bora;
(c) kutoa mapendekezo kwa kila Hadidu ya Rejea; na
(d) kuandaa na kuwasilisha Ripoti pamoja na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Sheria hiyo pia, inaainisha
Misingi ya Kitaifa na Maadili ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Tume katika
mchakato wa kupatikana Katiba Mpya. Misingi hiyo ni:
(a) kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) uwepo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
(e) umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(f) uchaguzi wa kidemokrasia na wa mara kwa mara katika vipindi
maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura;
(g) ukuzaji na uhifadhi wa Haki za Binadamu;
(h) utu, usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria; na
(i) uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na
inayoheshimu uhuru wa kuabudu.
Kwa ujumla, Sheria inaainisha
kazi na majukumu ya Tume kuwa ni:
(a) kuandaa na kuendesha programu za elimu kwa umma juu ya madhumuni
na majukumu ya Tume;
(b) kuitisha na kusimamia mikutano au Mabaraza ya Katiba katika
sehemu na nyakati mbalimbali kama
itakavyoamua;
(c) kutathmini na kuchambua maoni ya wananchi yanayokubaliana na yale
yasiyokubaliana; na
(d) kutayarisha na kuwasilisha Ripoti kwa kuzingatia Hadidu za Rejea.
Katika kutekeleza kazi na
majukumu yake, Tume imepewa mamlaka ya:
(a) kumtaka mtu yeyote, atakayehiari, kwenda mbele yake na kufanya
naye majadiliano kwa mazungumzo au kuwasilisha nyaraka;
(b) kupitia na kufanya uchambuzi wa michango, mawazo, maoni, taarifa
na mapendekezo yaliyotolewa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma, kupitia
nyaraka mbalimbali zilizoainishwa katika Sheria hiyo, na nyingine zozote ambazo
Tume itaona zinafaa;
(c) kumtaka Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za
Mitaa, Afisa Mtendaji wa Kata au Afisa Mtendaji wa Kijiji kuitisha mkutano wa
Wakazi wa Mji, Kata, Mtaa au Kijiji kwa Tanzania Bara;
(d) kumtaka Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa, Katibu wa
Halmashauri ya Mji au Wilaya, au Sheha kuitisha mkutano wa Wakazi wa Mji au
Shehia, kwa upande wa Zanzibar ;
(e) kuunda Kamati kwa ajili ya kazi za jumla au maalum;
(f) kumtumia au kumshirikisha mtaalamu mwelekezi au mtu yeyote kadri
itakavyokuwa lazima; na
(g) isipokuwa kama mazingira
yatahitaji vinginevyo, kutumia utaratibu unaofanana wa ukusanyaji na uchambuzi
wa maoni ya wananchi, uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba na uandaaji wa Ripoti.
Sheria pia imeainisha kuwepo
kwa Bunge Maalum la Katiba na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Aidha,
utaratibu wa kuwapata Viongozi na Sekretarieti ya Bunge Maalum la Katiba
umeainishwa katika Sheria hii. Sheria pia imeainisha utaratibu wa Bunge Maalum
kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na Utaratibu wa
Majadiliano ya kupitisha Rasimu ya Katiba itakayopendekezwa kwa Wananchi ili
kuipigia kura ya maoni. Katiba itapitishwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili
ya Wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wajumbe kutoka Zanzibar . Utaratibu wa
kura ya maoni na Uzinduzi wa Katiba mpya pia umeainishwa.
Kwa kifupi, Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ni Katiba au Msahafu wa Mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba unaoendelea hivi sasa. Sheria imeunda vyombo vyote muhimu
na kila chombo kimepewa hadidu za rejea. Kila chombo kimewekewa utaratibu wa
kazi na madaraka yake. Katika utaratibu huu kila chombo kina madaraka yake
yaliyowekewa mipaka. Haiyamkini kwa Tume kukusanya maoni, kuandika Rasimu ya
Katiba, kuiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba kisha nayo ishiriki
kuijadili Rasimu ya Katiba. Au, Bunge Maalum la Katiba, lenye madaraka ya
kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba wakati huo huo kuandika Rasimu ya Katiba
mbadala au kubadili mfumo wa Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Hivyo
hivyo, kwa Tume ya Uchaguzi na Wananchi. Kila aliyetajwa, ikiwa ni pamoja na
Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar ,
ana jukumu maalum lililoainishwa na Sheria.
4.0 WAPI TULIPO HIVI SASA
Kufuatia Tume kukabidhi
Ripoti na viambatanisho vyake kwa Marais, kama Sheria inavyoelekeza Rais
amekwishachapisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Gazeti la
Serikali na vyombo vingine vya habari, amekwishateua Wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba na kuliitisha Bunge Maalum la Katiba ili kukutana kuanzia tarehe 18
Februari, 2014, Dodoma .
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba atawasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum. Bunge hilo litakuwa na wajibu
wa kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba kabla ya kupigiwa kura ya maoni na
wananchi.
5.0 BUNGE MAALUM NA MAJUKUMU YAKE
Bunge Maalum la Katiba ni
chombo cha uwakilishi kama lilivyo Bunge la
kawaida isipokuwa Bunge Maalum la Katiba huundwa kwa ajili tu ya kutunga Katiba
na kufanya shughuli zingine zinazoambata na utungaji wa Katiba. Bunge Maalum la
Katiba hupewa jukumu hili la kutunga katiba badala ya Bunge la kawaida kwa
sababu Bunge Maalum la Katiba linawakilisha wananchi ambao ndio msingi wa
mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote ikiwemo Bunge la kawaida ambalo pia ni
zao la Katiba.
Majukumu ya Bunge la Maalum
la Katiba yanaweza kutofautina kulingana na namna utaratibu mzima wa mchakato
wa mabadiliko ya katiba ulivyopangwa. Katika baadhi ya nchi, Bunge Maalum la
Katiba hupewa mamlaka ya kusimamia mchakato wote wa mabadiliko ya katiba,
wakati katika nchi nyingine Bunge hili hushirikiana na vyombo vingine katika
kufanya na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba.
5.1 Madaraka ya Bunge Maalum
Madaraka ya Bunge Maalum
yamekuwa yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika kusini, Namibia na Cambodia Bunge Maalum
lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika Rasimu ya Katiba. Katika mazingira
haya, Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi katika
Rasimu ya Katiba. Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kuachana na Rasimu ya
Katiba na kuandika Rasimu Mbadala.
Madaraka ya Bunge Maalum
yanakuwa na mipaka endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Maadiliko ya
Katiba au Chombo cha aina hiyo. Bunge
Maalum linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye Rasimu
ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalum kubadili hoja ya msingi.
Jinsi ushirikishaji wa Wananchi unavyokuwa wa
wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalum yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia Bunge Maalum kunyang’anya
madaraka ya Wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Wataalam wa masuala ya Katiba, wanaeleza
kuwa madaraka ya Bunge Maalum katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya
Katiba.
Kwa mujibu wa kifungu cha
25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Bunge Maalum limepewa
madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba, kutunga Sheria ya
Masharti ya Mpito na Masharti yatokanayo na kabla ya kuanza kazi hiyo, Bunge
Maalum litapitisha Kanuni za Bunge Maalum ambazo zitaongoza utekelezaji wa
mamlaka ya Bunge Maalum.
5.2 Kanuni za Bunge Maalum
Kanuni za Bunge Maalum la
Katiba sharti zizingatie kwamba Bunge Maalum, kwa mujibu wa madaraka liliyopewa
chini ya kifungu cha 25(1) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ni chombo cha kuboresha masharti ya Rasimu ya
Katiba.
Katika kutekeleza madaraka ya
kujadili na kupitisha masharti ya kikatiba, Bunge Maalum litazingatia msingi
kwamba masharti ya kikatiba ndani ya Rasimu ya Katiba ni taswira, dira na ndoto
za Wananchi ambazo zimeelezwa kupitia maoni ya mwananchi mmoja mmoja na makundi
ya wananchi kupitia asasi, taasisi, jumuiya na makundi ya Watu Wenye Malengo
Yanayofanana.
Bunge Maalum litafanya kazi
ya kuboresha masharti ya Kikatiba yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo
kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha
masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
6.0 MUUNDO WA MUUNGANO WA
SERIKALI TATU
Muundo wa Muungano umewekwa
katika Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Ili kupata maana kamili ya muundo wa
Muungano unaopendekezwa, Tume ni vema kusoma Sura ya Kwanza ,
Sura ya Nane na Sura ya Kumi na tano.
Taswira ya Muungano wa
Serikali Tatu unaopendekezwa katika Rasimu ya Katiba imejengwa katika Ibara ya
1 inayoieleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuwa ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili – Sovereign Federal
Republic . Kwa hali hiyo
Muungano wa Serikali Tatu haubadili hadhi ya Jamhuri ya Muungano katika jumuiya
ya kimataifa kuwa ni nchi moja. Kupendekezwa kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika
haina maana ya kuunda nchi mpya. Kinachopendekezwa ni kutenganisha mamlaka ya
Mambo ya Muungano na Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika. Tanganyika na Zanzibar hazina hadhi ya
Jamhuri, na kwa hiyo si “Sovereign States” kama ilivyo Jamhuri ya Muungano.
6.1 Misingi ya Muundo wa Muungano wa
Serikali Tatu
Muungano wa Serikali Tatu
unaopendekezwa umezingatia mamlaka tatu zilizomo ndani ya Jamhuri ya Muungano
hivi sasa:
(a) Mamlaka ya Mambo ya
Muungano –Jurisdiction on Union Matters yanayosimamiwa na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 4(2), (3) na 34(1) na (3) za Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977;
(b) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar yanayosimamiwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984
na kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) na (3), 64(2) na (5) na Ibara ya 102 ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na
(c) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika ambayo kwa sasa
yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya sasa - Ibara ya 4,
34(2) na (3) na 64 (4).
Kila mamlaka sasa itakuwa na
Serikali yake ambayo itasimamiwa na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.
6.2 Mgawanyo wa majukumu na
madaraka katika Serikali tatu
Ibara ya 60 na Nyongeza ya
Kwanza inaorodhesha mambo saba ya Muungano ambayo yanasimamiwa na Jamhuri ya
Muungano. Haya ndiyo masuala makuu na ya msingi ya kidola (Sovereign Functions)
ambayo ndiyo yalivyo katika masuala 11 ya Muungano yaliyomo katika Hati ya
Muungano ya Mwaka 1964.
Katika mambo haya saba,
Jamhuri ya Muungano inayo mamlaka kamili tena yasiyogawanyika. Mambo hayo 7
hayawezi kufanywa na Serikali za Nchi Washirika wa Muungano kwa sababu hazina
sifa ya “Sovereign States”. Kwa mfano suala la ulinzi na usalama lipo moja kwa
moja katika Jamhuri ya Muungano. Pamoja na orodha ya mambo ya Muungano
yaliyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza, zipo taasisi ambazo zimetajwa
katika Rasimu ya Katiba kuwa za Muungano lakini hazijaorodheshwa. Taasisi hizo
na mambo hayo yamejumuishwa katika Mambo ya Muungano Yaliyokusudiwa katika aya
ya 1 ya Mambo ya Muungano, yaani – Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.
6.3 Hadhi ya Marais wanaotajwa katika Rasimu ya Katiba
Katika Rasimu ya Katiba yumo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar.
Ingawa wote wanaitwa Rais, lakini hawafanani kwa hadhi na majukumu. Rais mwenye
mamlaka juu ya Jamhuri ya Muungano ni Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo,
kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba, Rais wa
Jamhuri ya Muungano ndiye peke yake Mkuu
wa Nchi mwenye mamlaka kamili (Head of State), Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa
Serikali ya Muungano. Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar hawana sifa hizo
ingawa wao ni wakuu wa mambo yote yasiyo ya Muungano katika maeneo yao ya
utawala. Kwa kuhakikisha hilo, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar
hawakupewa hadhi ya Makamu wa Rais kwa makusudi. Kwa msingi huo hawawezi
kukaimu nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano akisafiri au akiwa hawezi
kutekeleza kazi kwa muda. Hilo likitokea wanaweza kukaimu ni Makamu wa Rais,
Waziri Mwandamizi, n.k.
6.4 Misingi ya utendaji ya Muungano wa Serikali Tatu
Muundo wa Serikali Tatu
umejengwa katika Misingi ya Utendaji (Principles) ifuatayo:
(a) Muungano wa Hiari (Voluntary Union);
(b) ushirikiano ( Co-operation);
(c) uratibu (Co-ordination);
(d) Mshikamano (Solidarity); na
(e) subsidiarity.
6.4.1 Muungano wa Hiari (Voluntary Union)
Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na iliyokuwa Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar. Msingi wa Muungano huu ni Makubaliano ya Muungano (Articles
of Union) ya mwaka 1964 yaliyofikiwa baina ya mataifa haya mawili. Chini ya
makubaliano hayo, mataifa hayo yalikubaliana kwa hiari kuachia baadhi ya
mamlaka na kuyapeleka mamlaka hayo katika Serikali ya Muungano. Uhiari huu wa
kukubali kuungana kwa mataifa haya mawili ni moja ya misingi ya utekelezaji wa
muundo wa Muungano unaopendekezwa wa Serikali Tatu. Ibara ya 1(3) ya Rasimu ya
Katiba inapendekeza pamoja na mambo mengine, Hati ya Muungano iwe ni msingi
mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
6.4.2 Ushirikiano (Co-operation)
Msingi mwingine wa utendaji
katika muundo wa Serikali Tatu ni Ushirikiano. Chini ya msingi huu, Serikali ya
Muungano na Serikali za Nchi Washirika zitakuwa na ushirikiano baina yao katika
shughuli zote za utendaji na uendeshaji wa nchi ili mradi ushirikiano huo
haukiuki Katiba. Ibara ya 65(1) inapendekeza kuwa Nchi Mshirika iweze kuomba
ushirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha
uhusiano wake wa kikanda au kimataifa. Aidha, Ibara ya 66 inapendekeza masharti
kuhusu ushirikiano kati ya Nchi Washirika zenyewe na baina ya Nchi hizo na
Serikali ya Muungano kwa lengo la kukuza na kulinda maslahi ya Taifa na kukuza
maendeleo ya wananchi.
6.4.3 Uratibu (Coordination)
Katika mfumo wa Serikali
Tatu, uratibu wa uhusiano baina ya Serikali hizo ni moja ya misingi muhimu.
Ibara ya 67 inapendekeza kuwepo kwa Waziri Mkaazi atakayeteuliwa na kila Nchi
Mshirika atakayefanya kazi akiwa Makao Makuu ya Serikali ya Muungano. Moja ya
majukumu ya msingi ya Waziri Mkaazi ni kuratibu uhusiano baina ya Serikali yake
na Serikali nyingine ya Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake na Serikali ya
Muungano. Aidha, Ibara ya 109 inapendekeza kuanzishwa kwa Tume ya Uhusiano na
Uratibu wa Serikali chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais. Kuwepo kwa uratibu
kutaimarisha uhusiano wa kiutendaji baina ya Serikali zinazopendekezwa na hivyo
kuimarisha Muungano.
6.4.4 Mshikamano (Solidarity)
Mshikamano (Solidarity) ni
moja ya misingi muhimu ya utendaji katika mfumo wa Shirikisho. Msingi huu
umezingatiwa katika Rasimu inayopendekezwa ili kuhakikisha kuwa Serikali zote
tatu zinashikamana na kusaidiana katika kila hali inayoweza kujitokeza. Mathalani,
Ibara ya 62(3) inapendekeza kuipa Serikali ya Muungano, kwa makubalino na
masharti maalum na Serikali ya Nchi Mshirika, madaraka ya kutekeleza jambo
lolote lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya Nchi Mshirika. Aidha, Ibara ya 65
na 66 zinapendekeza kuwepo kwa ushirikiano baina ya Serikali za Nchi washirika
na kati ya Serikali hizo na Serikali ya Muungano. Msingi huu ni muhimu katika
kuhakikisha kuwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano wananufaika kwa usawa
na mshikamano baina ya Nchi Washirika.
6.4.5 Subsidiarity
Msingi wa subsidiarity
unakusudia kuweka utaratibu wa mamlaka za chini kutekeleza majukumu yaliyo
ndani ya uwezo wake ikiwa mamlaka hizo zina uwezo wa kutekeleza majukumu hayo
kwa ukamilifu. Msingi huu wa subsidiarity unaruhusu mamlaka ya juu kutekeleza
jambo ambalo kwa kawaida hutekelezwa na mamlaka ya chini iwapo mamlaka ya juu
ina uwezo wa kutekeleza jambo husika kwa ufanisi au vinginevyo. Ibara ya 65 na
66 zimeweka msingi kwamba, ingawa Serikali ya Muungano itakuwa na mamlaka ya kushughulikia
Mambo ya Muungano, Serikali hiyo, kwa ridhaa ya Serikali ya Nchi Mshirika,
itakuwa na mamlaka ya kushughulikia masuala yasiyo ya Muungano katika Nchi
Mshirika. Msingi huu utasaidia kuimarisha utendaji katika muundo wa Serikali
Tatu unaopendekezwa.
6.5 Vyombo vya kikatiba vinapendekezwa kusimamia Misingi ya Utendaji
Katika kuhakikisha kuwa
Muungano unaimarika, Vyombo vipya vya kikatiba vimependekezwa kusimamia Misingi
ya Utendaji. Vyombo hivyo ni:
(a) Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali;
(b) Mawaziri Wakaazi;
(c) Mahakama ya Juu;
(d) Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
6.5.1 Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali
Tume ya Uratibu na Uhusiano
wa Serikali inaanzishwa na Ibara ya 109 na Makamu wa Rais atakuwa ndiye
Mwenyekiti wa Tume hii, na wajumbe wake
watakuwa ni Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar, Mawaziri Wakaazi na Waziri
mwenye dhamana ya mambo ya nje wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Tume hii,
pamoja na mambo mengine, itakuwa na dhima ya kusimamia na kuratibu uhusiano
baina ya Serikali za Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo na Serikali ya
Muungano. Tume hii ambayo inapendekezwa kuwa na Sekretarieti ya wataalam wa
fani mbalimbali, itakuwa pia na jukumu la kuwezesha uratibu na ushirikiano
katika kutekeleza masharti yanayopendekezwa na Rasimu ya Katiba, sera, sheria,
mipango na mikakati baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za
Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo.
6.5.2 Mawaziri Wakaazi
Waziri Mkaazi ni nafasi ya
madaraka inayopendekezwa na Ibara ya 67. Waziri Mkaazi atakuwa na wajibu wa
kuratibu na kusimamia uhusiano baina ya Serikali yake na Serikali nyingine ya
Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
6.5.3 Mahakama ya Juu
Mahakama ya Juu ni chombo
kingine kinachopendekezwa kuanzishwa katika Rasimu inayopendekezwa. Mahakama ya
Juu, pamoja na mambo mengine, inapendekezwa kuwa na mamlaka ya kushughulikia
kusikiliza na kuamua migogoro baina ya Nchi Washirika au baina ya Nchi Mshirika
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mamlaka haya ya Mahakama ya Juu yanakusudia
kusimamia misingi ya utendaji katika muundo wa Muunganounaopendekezwa
6.5.4 Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
Baraza la Ulinzi na Usalama
la Taifa linapendekezwa kuanzishwa na Ibara ya 237 ya Rasimu inayopendekezwa. Baadhi
ya Wajumbe wa Baraza hilo litaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ni
Makamu wa Rais, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar. Baraza hili litakuwa
ndicho chombo pekee kitakachowakutanisha Wakuu wa Serikali Tatu
zinazopendekezwa na kitakuwa chombo cha juu cha kusimamia misingi ya utendaji
katika muundo wa Serikali unaopendekezwa.
0 Comments