STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Februari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja ya Zanzibar na Ufaransa kuangalia maeneo mengine zaidi ya uhusiano ili kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo kwa manufaa ya pande mbili hizo.
Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na Ufaransa, kwa muda mrefu zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbali mbali ikiwemo elimu, miundombinu, utamaduni na sekta nyengine za kijamii, lakini kuna umuhimu mkubwa wa kupanua ushirikiano huo katika maeneo mengine.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Bwana Marcel Escure ofisini kwake ikulu Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema, ingawa Zanzibar imekuwa ikifanya vizuri katika sekta ya afya hasa katika kupunguza idadi ya vifo vya watoto, mama na wajawazito, lakini ni vyema kwa pande hizo mbili zikaliangalia kwa pamoja eneo hilo ili kuleta ufanisi zaidi ili hatimae Zanzibar iweze kufikia malengo yaliyowekwa kwenye Dira ya 2020, malengo ya milenia na MKUZA II.
Aidha, amesema eneo jengine ambalo pande hizo mbili zinaweza kushirikiana ni sekta ya utalii ambayo ni sekta kiongozi ya uchumi wa Zanzibar.
Kwa hivyo alisema ushirikiano kati ya Zanzibar na Ufaransa katika sekta hiyo ambapo Ufaransa inakaribishwa kuwekeza kwa kujenga mahoteli na kuleta watalii utazinufaisha nchi mbili hizo.
Dk Shein ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ufaransa kwa ushirikano inaoutoa katika sekta mbali mbali ikiwemo masomo ya lugha ya Kifaransa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar- SUZA.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Bwana Marcel Escure amesema nchi yake itaendelea kuziunga mkono jitihada za Serikali za kuleta maendeleo na kwamba Ufaransa pia inaangalia maeneo mengine zaidi ya ushirikiano na Zanzibar.
Aliongeza kuwa katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa upande wa sekta ya afya, Serikali ya Ufaransa inaangalia uwezekano wa kuanzisha huduma za afya kwa kutumia magari ili kuwafikia wananchi wengi zaidi maeneo ya vjijini.
Alisema hatua hiyo itaisaidia kuiwezesha Zanzibar kuharakisha kufikia malengo ya milenia hususan katika kuzidi kupunguza idadi ya vifo vya watoto, mama na waja wazito.
0 Comments