Na Masanja Mabula,Pemba
Vitambulisho 13,698 vya
Mzanzibari Mkaazi kutoka wilaya nne za Pemba, vimerejeshwa ofisi kuu Unguja,
baada ya kumaliza muda wake wa matumizi vikiwa katika ofisi za Pemba bila ya kuchukuliwa wa wahusika.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi, Ofisa wa Vitambulisho vya Mzanzibar Pemba, Hamad Shamata Hamad,
alisema kati ya vitambulisho hivyo 7,369 vinatoka mkoa wa kusini Pemba.
Alisema ofisi ya vitambulisho
imefikia uamuzi wa kuvirejesha ofisi kuu baada ya kukaa kwa muda mrefu na
wenyewe hawakujitokeza kuvichukua.
Alisema wilaya ya Chake Cheke
ndio inayoongoza kwa kuwa na vitambulisho vingi ikilinganishwa na wilaya
nyingine ambayo ilikuwa na vitambulisho 4,238 ikifuatiwa na wilaya ya Mkoani
iliyokuwa na vitambulisho 3,131.
Aidha alisema kuwa katika wilaya
ya Wete jumla ya vitambulisho 3,208 vimerejeshwa wakati vitambulisho 3,121
vimerejeshwa kutoka wilaya ya Micheweni.
Akitoa uchambuzi kimajimbo ,
Shamata alisema jimbo la Wawi ndio kinara likiwa na vitambulisho 1,349
likifuatiwa na jimbo la Chake Chake (1,079) na jimbo la Ziwani (1,004).
Kwa upande wa wilaya ya
Micheweni,jimbo la Konde ndilo linaloongoza kwa kuwa na vitambulisho 922 wakati
jimbo la Mkoani linaongoza kwa wilaya ya Mkoani kwa kuwa na vitambulisho 790
ambapo kwa wilaya ya Wete, jimbo la Wete linajumla ya vitambulisho 963.
Alisema wananchi ambao
vitambulisho vyao vimerejeshwa wakihitaji vitambulisho wanatakiwa kuanza taratibu
upya ikiwa ni pamoja na kuomba fomu kwa sheha wa shehia husika.
0 Comments