Na Mwashamba Juma
WAFANYAKAZI wa Shirika la
Magazeti ya Serikali, linalochapisha magazeti ya Zanzibar Leo, Zanzibar Leo
Jumapili na Zaspoti, wameaswa kujenga ushirikiano na udugu katika kufanikisha
majukumu ya kazi zao.
Wito huo ulitolewa jana na
Mhariri Mtendaji wa Shirika hilo, Abdulla Mohammed Juma, katika mkutano wa
wafanyakazi wa shirika hilo.
Alisema umoja na ushirikiano
hautopatikana katika maeneo ya kazi zao ikiwa wafanyakazi hawatothaminiana na
kuheshimiana kwenye utendaji wa kazi zao sambamba na kuwataka kila mmoja
kuheshimu kazi ya mwengine kwani kila kazi ina ugumu wake.
Akizungumzia baadhi ya
changamoto kwa idara za shirika hilo, aliwataka wakuu wa idara kufanya maamuzi
kisheria wanapotatua mizozo ya wafanyakazi wao badala ya kusikiliza malalamiko
ya upande mmoja.
“Kabla ya kufanya maamuzi ya
malalamiko ya wafanyakazi wetu, ni lazima tufanye mawasiliano nao ili tuamue
kisheria,” alifahamisha.
Nae Naibu Mhariri Mtendaji wa
Shirika hilo, Nasima Haji Chum, aliwaomba wafanyakazi kuepuka majungu badala
yake kufanyakazi kwa ushirikiano.
Aidha aliwataka kuepuka makundi yenye lengo la kuweka ubaguzi baina
yao.
Kwa upande wao wafanyakazi
waliwaomba viongozi wao kuimarisha mawasiliano baina yao ili kuepusha migogoro
ambayo ni chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo ya shirika hilo.
Waliwataka wakuu wa idara kuepuka
upendeleo baina ya wafanyakazi ili kuondosha matabaka, chuki na uhasama.
0 Comments