Na Hafsa Golo
JUMLA ya watoto 5,030
wameokolewa katika ajira mbaya na
kurejeshwa skuli katika maeneo tofauti Unguja na Pemba.
Aidha familia 920 zimeanzishiwa
miradi mbali mbali ili kuwaendeleza watoto wao kielimu.
Ofisa usimamizi wa mradi kutoka
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Sheikha Haji Dau,alisema hayo
katika ziara maalum ya kuangalia
mwenendo wa watoto hao kwa baadhi ya skuli wanazosoma.
Alisema watoto hao wana umri chini ya
miaka 18 na tayari walikuwa
wameacha masomo na kujishughulisha na ajira mbaya na wengine walikuwa kwenye hatari
ya kuingia katika ajira hizo.
Alisema watoto hao wametoka
katika shehia 45 za Unguja na Pemba na
miongoni mwa kazi walizokuwa wakizifanya
ni pamoja na kuvunja kokoto,kupara
samaki na kuvua,kukokota magari ya ngombe na kufanyakazi mahotelini.
Akizungumzia familia za watoto masikini zaidi
walioanzishiwa miradi, alisema lengo la kuanzisha miradi hiyo ni kuhakikisha
watoto hao wanapata haki ya msingi ya elimu.
Khalfan Abdalla (13) mkaazi wa Pwani Mchangani ambae miongoni mwa
wanafunzi waliookolewa katika ajira mbaya, aliliambia Zanzibar Leo kwamba
kutokana na ugumu wa maisha alilazimika kujishughilisha na kazi ya kupara
samaki ili kupata fedha za kusaidia familia yake.
“Nyumbani naishi na
bibi,nilikuwa nikienda Matemwe kupara samaki nikurudi nampa pesa bibi na kwa siku napara samaki 30 hadi 40 na kuna
siku nilichomwa na mwiba wa tasi nikaumia sana nikajishughulisha na kazi ya
nyengine,” alisema.
Nae Siliji Hamad Juma, alisema
mpango wa miradi kwa familia maskini umeweza kuwapunguzia ukali wa maisha na
kusaidia watoto wao kurejea skuli.
Mradi wa ajira za watoto unatekelezwa
na Mfuko wa Hifadhi ya Mtoto (Save the Children), Jumuia ya Kuharakisha Maendeleo
ya Wanawake Zanzibar (COWPZ),Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
(TAMWA), Jumuia ya Kupunguza Umasikini na Kuboresha hali za Wananchi kisiwani
Pemba (KUKHAWA ) na Jumuia ya Kupambana na Umasikini kisiwani Pemba, (PIRO) kwa
ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
0 Comments