Na.Aboud Hussein na Simai Mati
SERIKALI ya Zanzibar
inakabiliwa na upungufu mkubwa wa waauguzi wa afya ya akili katika hospitali kuu
ya wagonjwa wa akili ya Kidongochekundu, hali inayosababisha wagonjwa kupata
huduma za chini mno.
Hilo limebainishwa jana na
Ofisa wa Ustawi wa Jamii, ambaye pia ni Muunguzi katika kituo hicho, Saghira
Mohammed Abdallah, wakati akizungumza na Zanzibar Leo, katika hospitali ya kuu
ya wagonjwa wa akili ya Kidongchekundu mjini Unguja.
Alisema suala la wauguzi na
tatizo la usafiri katika hospitali hiyo,ni moja ya changamoto kubwa
inayoendelea kuwasumbua katika utoaji wa huduma.
Alisema kituo hicho kwa sasa
kina wauguzi wanne, ambapo kwa uwiano kila muuguzi mmoja anahudumia karibu
wagonjwa 100 kwa siku, badala ya muuguzi mmoja kuwahudumia wagojwa 20.
Kwa upande wa usafiri, alisema
hospitali hiyo ina gari moja ambapo inapokosa mafuta kazi zinashindwa
kufanyika.
Aidha alisema hospitali
inakabiliwa na uhaba wa dawa hasa kwa wagonjwa wa nje hali inayosababisha
matatizo kwa wagonjwa wa akili kuongezeka.
Alisema kila kidonge kimoja aina
ya carbamazipine kina gharimu shilingi 200, ambapo mgonjwa mmoja anatakiwa
kutumia mara tatu kwa siku, jambo ambalo humfanya mgonjwa kutumia takribani shilingi 1000
kwa siku.
Kwa ujumla alisema
hospitali inakabiliwa na tatizo la kutoa matibabu bora kwa wagonjwa wa akili.
Nae Mratibu wa Afya ya Akili ya
Jamii Kanda ya Unguja, Mohammed Joel, alisema tatizo la ugonjwa wa akili
limekuwa kubwa Zanzibar na linasababishwa kwa kiasi kikubwa na matatizo ya
kimazingira, kimwili na kijamii kama vile urithi, utumiaji wa dawa za kulevya
na hali ngumu za maisha.
Alitoa wito kwa wanajamii na
kwa wadau wengine kutokuwachukulia vibaya au kuwanyanyapaa wagonjwa wa afya ya
akili, kwani kila mmoja anaweza kukutwa na ugonjwa huo katika mazingira
tofauti, na sio lazima atumie dawa za kulevya.
Hospitali ya wagonjwa wa akili
kwa sasa ipo kwenye maadhimisho ya siku ya wagonjwa wa akili duniani ambayo
hudhimishwa Oktoba 10 kila mwaka.
Katika maadhimisho hayo kituo
hicho kimeendesha shughuli mbalimbali tangu Oktoba mosi, zikiwemo usafi wa
mazingira, darasa kwa wagonjwa wa nje, ziara za kiafya, kutoa elimu kupitia
vyombo vya habari na kilele chake kitaambatana na michezo ya aina mbalimbali
kwa wagonjwa.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni
‘Kuishi na Skizofrenia’ (Living with Schizophrenia), inayomaanisha akili kuwa
na mitazamo hasi na kutokujielewa katika hali ya kawaida, ambapo Shirika la Afya
Ulimwenguni limeiweka kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanajamii kuishi na hali
hiyo kwa usalama.
Kwa mujibu wa WHO, asilimia 26
ya watu wote ulimwenguni wanasumbuliwa na skizofrenia, asilimia 50 ya wagonjwa
hawatibiki, kutokana na ugonjwa huo, na asilimia 90 ya wagonjwa wote ni kutoka
katika nchi zinazoendelea.
0 Comments