Na Rose Chapewa, Mwanza
JESHI la polisi mkoani Mbeya
limeelezea kusikitishwa na habari ya uchochezi
iliyoandikwa na chombo kimoja cha
habari, ikidai jeshi hilo litakifanyia kitu kibaya Chama cha Demokrasi na
Mendeleo na kudai habari hizo zina lengo la kuligombanisha jeshi hilo na chama
hicho.
Hayo yalibainishwa na Kamanda
wa polisi mkoa huo, Ahmed Msangi, wakati
akizungumza na waandishi wa habari na
kuwashukuru kwa kufika ofisini kwake
kupata ufafanuzi na hivyo kuzingatia misingi na maadili ya uandishi ya kuandika
habari sizoegemea upande mmoja, baada ya uongozi wa Chadema mkoa wa Mbeya,
ukiongozwa na Mbunge wa jimbo la Mbeya, Joseph Mbilinyi, kulalamikia kauli
hiyo.
Alisema habari hizo ni za
uchochezi na zenye lengo la kuharibu uhusiano uliopo kati ya viongozi wa vyama
vya siasa ikiwemo Chadema.
Alifafanua kuwa yeye ni
kiongozi anayewatumikia wananchi wote na kwamba kiongozi yeyote mwenye maadili
ya utumishi hawezi kusema kitu kama hicho huku akiwapa pole viongozi wa Chadema
kwa habari hiyo ambayo imewaumiza.
“Hiyo habari nami pia nimeisoma
kwenye gazeti, na baada ya kuiona nilimpigia simu mwandishi aliyeiandika na
nikamwambia sijapenda kuandika kitu ambacho sikukisema, na pia hata bosi wake
wa hapa Mbeya naye nilimweleza,” alisema.
Awali uongozi wa Chadema mkoa wa Mbeya,
uliitisha mkutano wa pamoja na vyombo vya habari, ukimtaka Kamanda
Msangi, kukanusha taarifa iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku la Kiswahili
nchini, kuwa atakifanyia kitu kibaya chama hicho.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana
la Chadema, John Mwambigija, alisema kutokana na kauli hiyo chama kimejipanga
kuhakikisha kinakabiliana na tatizo lolote litakalosababishwa na jeshi la
polisi.
Alisema wanachama wa Chadema
hawaliogopi jeshi la polisi, na kutoa siku tatu kwa kamanda wa polisi mkoa huo,
kukanusha taarifa hizo.
“Sisi tuna taarifa za kiusalama
kama wao wanavyosema tunapata taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi, na
tayari tumeshawaagiza vijana wetu, wanawajua polisi walioko uraiani, kama
hatafuta kauli yake tutawaambia polisi walioko uraiani waende wakakae nyumba za
polisi,” alisema.
Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph
Mbilinyi, alisema anasikitishwa na kauli ya kiongozi huyo aliyepewa dhamana na jeshi
la polisi, na kumuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Mkuu wa
Jeshi la Polisi, Ernest Mangu, kumfuta kazi mara moja.
Alisema kauli hiyo ya vitisho
si kwa ajili ya wanachama wa Chadema tu
bali inaathiri wananchi wote wa mkoa wa Mbeya, huku akijigamba kuwa wakazi wote wa Mbeya ni wanachama wa Chadema.
0 Comments