
STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS
RELEASE
Zanzibar 01 Novemba,2014
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar itahakikisha inaiendeleza sekta ya michezo sambamba na kuimarisha miundombinu yake ili
Zanzibar iweze kurejesha hadhi yake katika sekta hiyo.
Dk.
Shein aliyasema hayo, leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye sherehe za
ushindi wa michezo mbali mbali ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM,
zilizofanyika huko katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar ambazo pia,zimehudhuriwa
na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi
mbali mbali wa serikali wanamichezo na wananchi.
Katika
hotuba yake hiyo, Dk. Shein alisema kuwa katika kufanya hivyo, Serikali
inapitia upya Sera ya Michezo ili iweze kufikia malengo ya Serikali katika
kuinua sekta ya michezo hapa nchini.
Alisema
kuwa wakati mchakato wa kuipitia upya Sera ya Michezo ukiendelea
aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea na juhudi zake za kuimarisha
miundombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja mbali mbali vya michezo Unguja
na Pemba.
Dk.
Shein alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanja vitatu vya
Kimataifa hapa Zanzibar vinaimarishwa ambapo hivi sasa tayari uwanja wa Amaan
uliopo mjini Unguja uko tayari na kiwanja cha Gombani Pemba tayari kimeshajegwa
ambacho ndani ya mwaka huu wa fedha uwanja huo utawekwa tatan katika eneo la
kukimbilia.
Aidha,
Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeshafikia makubaliano na Serikali ya Jamhuri
ya Watu wa China ya ujenzi wa uwanja wa Mao-te-tung ili nao uweze kutumika
sambamba na viwanja vya Amaan na Gombani huku akieleza azma ya kuviimarisha
viwanja vyengine mbali mbali vya Unguja na Pemba kwa lengo la kuendeleza
michezo pamoja na kutoa fursa nzuri kwa wananchi waweze kuendeleza michezo kwa
ufanisi zaidi hapa Zanzibar
Dk.
Shein alipendekeza kuongezwa kwa mashindano ya mpira wa miguu ili kuleta
ushindani katika vilabu vya mpira vya hapa Zanzibar pamoja na kuvishirikisha
vilabu vyengine kadhaa.
Alisema
kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuzijengea uwezo timu za
Zanzibar ili ziweze kushiriki mashinadano ya ndani na nje ya nchi na kupata mafanikio na kusisitiza kuwa wakati
umefika Zanzibar kuwa mshindani katika mashindano na kuchukua vikombe katika
mashindano mbali mbali.
Dk.
Shein alisema kuwa Zanzibar ina vipaji vya kutosha na wanamichezo wa kufanya
vizuri wapo, kinachotakiwa ni maandalizi bora na kuondoa migogoro katika
uongozi wa vilabu na vyama vya michezo hapa Zanzibar.
Kwa
kusisitiza hilo, Dk. Shein alitoa mfano wa mgogoro wa Chama Cha Mpira wa Miguu
Zanzibar (ZFA) katika uongozi uliopita ambapo ulisababisha wanamichezo wa timu
ya Taifa ya Zanzibar walioshiriki katika mashindano ya 'Challange Cup' mwaka juzi
kushindwa kuwakabidhi zawadi aliyowaandalia kutokana na migogoro kadhaa ndani
ya chama hicho.
Alieleza
kuwa iwapo mashirikiano mazuri yatakuwepo sekta ya michezo itapata mafanikio
makubwa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa malengo yake ya
kukuza sekta ya michezo nchini yanafanikiwa.
Dk.
Shein alisema kuwa michezo ni afya,
ukakamavu, inajenga udugu na kuleta ushirikiano na kwa hivi sasa, michezo ni
ajira kwa hivyo ni vyema wananchi wote wakashiriki katika michezo japo ya
vilabu vya mazoezi ili kuimarisha afya zao.
Aidha,
Dk. Shein alieleza kuridhishwa sana na mafanikio ya timu ya mpira wa miguu ya
KMKM kwa kuwa mabingwa kwa misimu miwili mfululizo 2013-2014 na 2014-2015 pamoja
na ushindi wa timu ya riadha pamoja na
kupata ngao za hisani. "Naungana na nyinyi na wale wote wanaokupongezeni
kwa mafanikio hayo", alisema Dk. Shein.
"Napenda
kuwapongeza wanamichezo wa KMKM kwa kuchagua mbio hizi ambazo kwa kweli
zinatukumbusha na sisi wengine enzi zetu katika michezo ya riadha hasa ya
'cross-country na field tract' tulishiriki vyema pamoja na mchezo huu wa
kuvuta kamba ambapo mimi mwenyewe nilikuwa kocha", alisema Dk. Shein.
Alisema
kuwa Uongozi wa Awamu ya Kwanza ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ulichukua
jitihada za makusudi kujenga Uwanja wa Amaan uliofunguliwa mwaka 1970 na ule wa
Gombani uliofunguliwa mnamo mwaka 1992 wakati wa uongozi wa Awamu ya Tano
ambapo ujenzi wake ulianza katika uongozi wa Awamu ya Nne chini ya Marehemu
Sheikh Idrisa Abdul Wakil.
Dk.
Shein vile vile, alisisitiza haja ya kila timu hapa Zanzibar kuwa na Klabu yake
na jengo lake na kuunga mkono azma ya klabu ya KMKM kutaka kujenga jengo maalum
la ghorofa litakalokuwa na eneo la kufanyia mazoezi (GYM), ukumbi wa mikutano
na maduka ya vifaa vya michezo.
Mapema
Dk. Shein aliyapokea mashindano ya mbio
za kilomita kumi katika viwanja hivyo vya Maisara yalioanzia huko Kibweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, na
kuwashirikisha wakimbiaji zaidi ya 200 ambapo
mkimbiaji Philip Jacob Mambo kutoka
Kikosi cha Mafunzo aliibuka mshindi wa kwanza na Mohamed Ramadhan kutoka KMKM
ambae aliibuka mshindi wa Pili.
Kwa
upande wa wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Albina Edward kutoka KMKM na mshindi
wa pili alikuwa Nuru Nasib kutoka Kambi ya Mtoni. Mashindano hayo pia,
yalijumuisha Makundi maalum ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mkimbiaji
Ali Abdalla na mshindi wa pili alikuwa Amina Daudi Simba.
Nae
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji
Omar Kheir alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kushirikiana pamoja na wanamichezo
hao wa Kikosi cha KMKM katika sherehe zao hizo.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mkuu wa KMKM Komodoo Hassan Mussa alisema kuwa mbio za
kilomita 10 ambazo zilishirikisha wanamichezo zaidi ya 200 zimefanyika kwa mara
ya kwanza mwaka huu lakini zitafanyika kila mwaka katika siku itakayoteuliwa
kuwa ya KMKM.
Katika
risala yao nao wanamichezo wa KMKM walieleza mikakati inayochukiliwa katika
kuendeleza michezo katika kikosi chao sambamba na kupongeza jinsi Serikali
inavyowaunga mkono katika kufikia malengo waliyojiwekea
Sherehe
hizo ziliambatana na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya sanaa vikiwemo Diamond
Morden Taarab, Kidumbaki kilichoongozwa na Msani Makame Faki maarufu sauti ya
zege, ngoma ya Kibati kutoka kikundi cha sanaa cha JKU, JKU Morden Taarab ambacho
kiliimba wimbo maalum kwa ajili ya sherehe hiyo.
Pia, mchezo wa
kuvuta kamba ulifanyika katika sherehe hizo ambao uliwashirikisha
maafisa wa KMKM wanaofanya kazi pamoja na Wastaafu ambapo Wastaafu walipata
ushindi na kukabidhiwa zawadi na Rais zikiwemo fedha taslim zilizotolewa na
wapenda michezo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 Comments