6/recent/ticker-posts

Balozi wa COMORO NCHINI akutana na Rais Dk.Shein,Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi wa Comoro Nchini Tanzania Dk.Ahamada El Badaoui  Mohamed alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa mazungumzo na Rais
  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Balozi wa Comoro Nchini Tanzania Dk.Ahamada El Badaoui  Mohamed alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana  na  Balozi wa Comoro Nchini Tanzania Dk.Ahamada El Badaoui  Mohamed baada ya mazungumzo yao leo  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar
   Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na  Balozi wa Comoro Nchini Tanzania Dk.Ahamada El Badaoui  Mohamed baada ya mazungumzo yao leo  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,[Picha na Ikulu.]


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                           7.1.2015
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisistiza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Comoro hasa katika uimarishaji wa sekta za maendeleo na utamaduni.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Comoro nchini Tanzania Dk. Ahmada El Badaoui Mohamed, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano huo wa muda mrefu sambamba na maingiliano na uhusiano wa watu wake kati ya nchi mbili hizo ambao wameweza kuimarisha udugu wao wa kihistoria.

Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alisema kuwa mashirikiano katika uimarishaji wa sekta za maendeleo sambamba na utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano uliotiwa saini hapo mwaka jana wakati wa  ziara yake aliyoifanya nchini humo utasaidia kuimarisha juhudi hizo.


Dk. Shein alisema kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Comoro ambao umeweza kukuza udugu miongoni mwa watu wake.

Mbali ya uhusiano huo wa kimaendeleo kati ya Zanzibar na Comoro, Dk. Shein alisema kuwa nchi mbili hizo zimekuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu katika kukuza mila na tamaduni  zake sambamba na mafunzo hasa katika elimu ya dini ya Kiislamu.

Alisisitiza kuwa mashirikiano katika sekta ya elimu, habari,biashara, usafiri na usafirishaji  pamoja na sekta nyenginezo utazidi kuimarisha uhusiano wa Comoro na Zanzibar ambao ni wa muda mrefu.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo wa Comoro juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kupambana na kupiga vita uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini kwa kutambua changamoto zilizopo kwa nchi za visiwa.

Nae Balozi wa Comoro nchini Tanzania Dk. Ahmada El Badaoui Mohamed alisema kuwa Comoro inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake na Zanzibar ambao nchi yake umeahidi kuudumisha kwa manufaa ya pande zote mbili.

Balozi huyo alisema kuwa Comoro na Zanzibar ina historia kubwa katika kutoa elimu hasa ya dini ya Kiislamu na kueleza kuwa mashekhe wengi wakubwa wa Comoro elimu yao hiyo wameipata hapa Zanzibar akiwemo baba yake mzazi.

Alisema kuwa Comoro inajivuinia kwa hilo na kusisitiza kuwa ipo haja kwa viongozi wa dini wa nchi mbili hizi kuzidisha mashirikiano na kukuza uhusiano ikiwa ni pamoja na kutembeleana na kubadilishana uzoefu katika elimu ya dini ya Kiislamu.

Aidha, Dk. Ahmada alisema kuwa utekelezaji wa mkataba wa makubaliano uliosainiwa katika ziara ya Dk. Shein aliyoifanya nchini humo mwaka jana utasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliokusudiwa katika uimarishaji wa sekta za maendeleo na ukuzaji wa uchumi kwa pande zote mbili.

Pamoja na hayo, Balozi huyo alieleza faraja atakayoipata yeye binafsi pamoja na nchi yake katika utekelezaji wa moja ya makubaliano hayo ambayo ni kuimarisha lugha ya kiswahili nchini humo kutokana na mashirikiano na taasisi husika ya hapa Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Post a Comment

0 Comments