6/recent/ticker-posts

Tanzania Yataka Mashirika ya Umoja wa Mataifa Kutekeleza kwa Vitendo Dhana ya Uwazi na Uwajibikaji.

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  katika Umoja wa  Mataifa, Balozi Tuvako Manongi (picha ya Maktaba) ametoa wito  kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Ofisi zake kutekeleza kwa   vitendo dhana ya uwazi na uwajibikaji kama  yanavyozishinikiza  Nchi Wanachama, kwa kile alichosema, utekelezaji wa dhana hiyo haupashwi kuwa ni jukumu la Serikali  peke yake.Ametoa wito huo wakati wa  majadilino ya Ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu iliyowasilishwa  mbele ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya  jumatatu

Na MwandishiMaalum,  New York

Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania,  imetoa wito kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, ikiwamo Baraza la Haki za Binadamu kuitekeleza kwa vitendo dhana ya uwazi na uwajibikaji.

Tanzania imesisitiza pia kwamba,   haitoshi kwa Mashirika hayo kuzitaka nchi wanachama kwa maana ya serikali kuwajibika na kuwa wazi katika utekelezaji wa majukumu yake ili hali yenyewe yanafanya kinyume.

Wito huo umetolewa siku ya Jumatatu na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katikaUmoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi,  wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  lilipokea na kujadili Ripoti ya Mwaka ya Baraza la Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Balozi Manongi ambaye alikuwa miongoni mwa Mabalozi kati ya wengi waliochangia Ripoti hiyo iliyowasilishwa na Rais wa Baraza la  Haki za Binadamu Bw .Joachim Rucker. Amesema,  Tanzania  inatoa wito huo kutoka kile kinachoonekana dhahiri kwamba ama Mashirika hayo yamekuwa yakionyesha kuegemea upande mmoja dhidi ya mwingine   au  kupendelea nchi moja dhidi ya nyingine kitendo ambacho kinakwenda kinyume na kile wanachokihubiri.

Akatoa mfano kwa kusema, wakati Rais wa Baraza la  Haki za Binadamu akisisitiza katika ripoti yake umuhimu wa uwajibikaji, Ofisi ya Haki za Binadamu katika mwezi Octoba ikishirikiana na  UNICEF na  Canada,  ilidhamini onyesho la Filamu kuhusu kijana kutoka Geita mwenye alibinisim,  pasipo Taasisi hiyo kuujulisha Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania ili hali wakijua Tanzania ilikuwa mlengwa wa filamu hiyo.

“Akiwasilisha Taarifa yake mbele ya Baraza hili mwanzoni mwa mkutao huu, Rais wa Baraza la  Haki za Binadamu amesisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji. Cha  kusikitisha tukio la konyeshwa kwa filamu ambayo maudhui yake yalihusu Tanzania na sisi kama Tanzania hatukujulishwa, hakika inakwenda kinyume kabisa na dhana ambayo Rais wa Baraza la  Haki za Binadamu amekizungumza hapa” akasema Balozi Manongi


Na kuongeza“ ndiyo maana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa wito kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa au Ofisi zake kuonyesha kwa vitendo dhana ya uwazi,   uwajibikaji na kutoegemea upande wowote”.

Akabainisha kuwa,  Mashirika ya Umoja wa Mataifa hayapashwi kujionyesha kuwa yanaegemea upande wowote au hata kupendelea baadhi ya nchi wanachama dhidi nchi nyingine na hasa  pale ambapo Mashirika hayo binafsi hayajapitia na kujiridhisha juu ya kile ambacho wanataka kukiunga mkono  au  kutaka kujihusisha  nacho.

Akaeleza Zaidi  mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba,  Tanzania  haikupinga na wala haipingi filamu kuhusu kijana wa Geita,  filamu iliyolenga katika kuonyesha changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino nchini Tanzania

“ Tulichopinga na tunachopinga ni maelezo yaliyoandikwa na muandaaji wa filamu hiyo, maelezo ambayo yalikuwa na upotoshaji mkubwa. Kwa mfano,baadhi ya maelezo ya filamu hiyo yanasema, hakuna utashi wa kisiasa kutoka Serikali ya Tanzania  katika kukabili uovu wanaotendewa watu wenye ualibino. Kwamba, msukumo kutoka mataifa ya nje ni walazima ili kutokomeza uovu huo,  kwamba ujinga ni laana kubwa inayowakabili waaafrika na jawabu pekee ni kuwaelimisha, kwamba filamu hiyo ilikuwa ni kuwashawishi watu wanje ili kuleta mabadiliko ya kweli.

Na  vile vile filamu hiyo ilikuwa ni kusherehekea roho ya utu na kazi nzuri inayofanywa na watu wa Canada katika kuwasaidia watu wenye ualibino” akasisitiza Balozi Manongi

Akasema Balozi, Ni kwa kuzingatia upotoshaji huo na mwingine ulioelezwa na muandaaji wa filamu hiyo, haishangazi kuona kwamba Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  haukualikwa kufadhili onyesho la filamu hiyo iliyoonyeshwa Umoja wa Mataifa.

“ Rais wa Baraza la Haki za Binadamu pia amezungumzia wajibu wa Asasi za Kijamii katika uhamasishaji wa haki za Binadamu.  Tunakubaliana na pendekezo wake. 

Wakati tunauga mkono mchango wa Asasi za kijamii, nilazima basi Asasi hizo nazo zikaonyesha uwajibikaji na uwazi pamoja na kujipambanua katika utekelezaji wa majukumu yao.

Uwajibikaji hauwezi kuwa ni jukumu la serikali peke yake” akasisitiza Balozi Manongi.

Akizungumzia Zaidi kuhusu changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino, Mwakilishi huyo wa Tanzania, amesema,  Tanzania  kwa kutambua changamoto kubwa za kijamii na kiuchumi pamoja na upatikanaji wa haki za msingi kwa watu wenye ualibino ndiyo maana kwa kushirikiana na  Malawi   imeamua kuwasilisha mbele ya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la   Umoja wa Mataifa Azimio kuhusu watu wenye ualibino.

Amesema dhumuni kuu la Azimio hilo na ambalo linatarajiwa kupitishwa wiki hii ni kupanua wigo na ushiriki mpana wa wadau mbali mbali ukiwamo Umoja wa Mataifa katika kuzikabili changamaoto zinazowakabili watu wenye ualibino.

Na kwa sababu hiyo, Balozi Manongi ameziomba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa,  kuunga mkono azimio hilo pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania pamoja na  Chama cha Watu wenye Ualibino Tanzania (TAS) katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino vikiwamo vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa na watu wasio na mapenzi mema.

Post a Comment

0 Comments