Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Sekta binafsi itahakikisha kuwa Sekta ya Uwekezaji inazidi kukuwa na kuimarika zaidi nchini.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla katika uzinduzi wa mradi wa hoteli ya Matemwe Attitude iliyopo Kijini Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kuimarika kwa sekta ya uwekezaji ndiko kunakowavutia wawekezaji kuendelea kuekeza kwa wingi zanzibar jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ajira kwa wananchi wazawa na kukuza uchumi kwa jamii inayowazunguka.
Amefahamisha kuwa jitihada hizo zimetoa matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji katika Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Utalii, Ujenzi, Nishati na kuzalisha fursa nyingi za ajira ambapo Takwimu za Serikali zinaoesha kuwa zaidi ya miradi ya uwekezaji 588 imesajiliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani Billioni 6.9 na kuweza kuzalisha ajira zaidi 28,695 kwa wazawa.
Amesema amefurahishwa na kauli ya muekezaji wa Hoteli ya Matenwe Attitude kuahidi kuwa kipaombele chao kitakuwa ni kuhakikisha wanaweka mazingira bora katika maeneo yanayowazunguka sambamba na kuigusa jamii moja kwa moja katika nyanja mbali mbali lengo ni kuhakikisha ustawi bora wa wananchi wa Kijini na Mkoa wa Kaskazi kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Hemed amesema Serikali itaendelea kuweka mzingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji ili waendelee kuja kuekeza Zanzibar ambapo amewasisitiza wananchi kutoa usirikiano kwa wawekezaji sambamba na kulinda mila, silka na Tamaduni za kizanzibari.
Makamu wa Pili wa Rais amewataka wananchi walioajiriwa hotelini hapo kufanya kazi kwa umakini, Uadilifu na kufuata sheria za kazi pamoja na maelekezo ya waajiri wao.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikano, kuyalinda, kuyadumisha na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ili kuendelea kupata maendeleo nchini.
Nae, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar Mhe. Sharifa Ali Sharifa amesema Serikali kupitia Wizara ya kazi na uwekezaji inaandaa kanuni ya ushirikiano na uwajibikaji katika jamii ambayo itawabana wawekezaji waweze kujisogeza katika jamii wanayowekeza miradi mbali mbali ili nao waweze kunufaika na uwekezaji unaofanyika katika marneo yao.
Mhe. Sharifa amesema atahakikisha wafanyakazi wa ZIPA wanafanya kazi kwa wakati na weledi mkubwa kwa viwango vinavyotakiwa ili kuhakikisha sekta ya uwekezaji inazidi kukua Zanzibar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli ya Matenwe ATTITUDE Bwana RAVIN UNTHIAH amesema wameamua kuekeza Zanzibar kutokana na Amani na utulivu uliopo, Mazingira mazuri ya Uwekezaji na wananchi kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji jambo linalopelekea mazingira ya uwekezeji kuwa rafiki na wezeshi kwa waeekezaji wanaowekeza Zanzibar.
RAVIN amefahamisha kuwa kuzinduliwa kwa hoteli hio kutatoa fursa ya ajira zaidi ya 190 kwa wananchi wa Kijini na Mkoa wa Kaskazini kwa ujumla ambapo wafanyakazi hao tayari wameshapatiwa mafunzo na ujuzi kulingana na kada zao wanazozifanyia kazi ili waweze kutoa huduma bora kwa wageni na wazawa watakaofika hotelini hapo.
Amesema Matemwe Attitude group ina zaidi ya hoteli tisa(9)zenye madaraja tofauti ambapo licha ya uwekezaji huo Matemwe Attitude group kwa kushirikiana na Serikali wamelenga kusaidia katika kukuza uchumi na kuisadia jamii iliyowazunguka katika nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 31 / 12 / 2025
0 Comments