6/recent/ticker-posts

Suala la Makazi Bora Limeendelea Kupewa Kipaumbele na Serikali Ili Kuwawezesha Wananchi Kuishi Katika Mazingira Salama

NA MWAJUMA JUMA 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Idrissa Mustafa Kitwana, amesema suala la makazi bora limeendelea kupewa kipaumbele na serikali ili kuwawezesha wananchi kuishi katika mazingira salama na yenye staha, sambamba na kulinda misingi na dira ya viongozi waliotangulia.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi na biashara uliofanyika Chumbuni, Unguja, Waziri Kitwana alisema mradi huo ni uthibitisho wa dhamira ya serikali katika kutekeleza kwa vitendo malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar, yenye lengo la kuimarisha maisha ya wananchi.

Alisema kuwa hatua hiyo inadhihirisha muendelezo wa falsafa ya Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, aliyedhamiria kuona wananchi wake wanapata makazi bora na huduma muhimu kwa maendeleo ya jamii.

Waziri Kitwana, aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mstaafu, Balozi Seif Ali Iddi, alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Zanzibar imeendelea kuheshimiwa na kupiga hatua katika sekta ya makazi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nyumba za gharama nafuu kwa wananchi.

Alifafanua kuwa katika kufanikisha azma hiyo, serikali imekuwa ikichukua jitihada madhubuti, ikiwemo kutenga bajeti maalumu na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa makazi bora yanayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Aidha, Waziri Kitwana alisisitiza umuhimu wa wadau wote kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan sekta ya makazi, ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) Sultan Said alisema ujenzi wa nyumba hizo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimakakati inayotekelezwa  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha alisema kuwa mradi huo  unatekelezwa chini ya maono ya  serikali  ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussain Ali Mwinyi ambae alisisitiza umuhimu wa kuimarisha makaazi ya wananchi.

Hata hivyo alisema kuwa  mradi huo utahusisha nyumba 3000 ambapo kwa  awamu ya kwanza watajenga nyumba 1500 kwa gharama ya zaidi ya shilingi  milioni 144 katika hatua za awali  ikiwemo ujenzi wa ukuta, miundombinu ya maji na umeme na miundombinu mengine.

Alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo una mafanikio makubwa kwa wananchi hasa kulingana na maelekezo ya rais asilimia 40 zimewekwa kwa ajili ya kuwapangisha wananchi wanyonge wasio na uwezo uhaulishaji wa wananchi.

Nae Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar  Salha Mwinjuma mradi wa huo  unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa eneo hilo, kuongeza ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi, huku ukizingatia upangaji bora wa miji na maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Aidha aliwashukuru wananchi kwa kuhudhuria katika shughuli hiyo na ishara hiyo inaonesha kwamba wameupokea mradi huo.

Alisema mradi huo ni mkakati na.kupitia hilo wanamshukuru mkurugenzi mkuu kwa kuwaheshimisha katika kufanikisha mradi huo na kuwataka wananchi wanedelee kuwaunga mkono kwa muda wote wa ujenzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Talib Ali Talib alisema kuwa.anachokifanya Dk.  Mwinyi ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo inaelekeza makaazi bora kwa wananchi.

Hata hivyo alisema kuwa kwa kasi ambayo anaionesha rais Mwinyi wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika shughuli zote za kimaendeleo na kumsemea kwa wengine.

Sambamba na hayo aliwahimiza wananchi kuendelea kuilinda amani na.utulivu ili kumpa nafasi zaidi ya kuendelea kuwaletea maendeleo nchini.

Post a Comment

0 Comments