Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akiiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendelea kuongeza udhibiti wa mikopo yenye riba kubwa (mikopo umiza) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Mhe. Dkt. Neema Peter Majule, aliyetaka kufahamu Serikali imechukua hatua gani kwa watu ambao wamejinufaisha kwa mikopo yenye riba kubwa, bungeni jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Fedha)
Na. Peter Haule, WF, Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula
(Mb) ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuendelea
kuongeza udhibiti wa mikopo yenye riba kubwa (mikopo
umiza) ili wananchi wapate mikopo yenye tija.
Ametoa maagizo hayo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu
swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Dkt.
Neema Peter Majule, aliyetaka kufahamu hatua
zilizochukuliwa na Serikali kwa watu wanaojinufaisha kwa
kutoza riba kubwa kwenye mikopo, hatua inayopunguza
jitihada za Serikali za kuwakwamua wananchi kiuchumi
hususani wanawake na vijana.
Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali imeanza kuchukua
hatua kwa wote wanaokiuka taratibu zilizowekwa na Serikali
za utoaji mikopo kwa kusitisha leseni zao na hatua nyingine za
kisheria.
“Wizara ya Fedha imejipanga kuhakikisha taasisi zote
zinazotoa mikopo zinafuata taratibu na tayari Serikali
imeandaa rasimu ya kusimamia mikopo ya kidigitali
inayotarajiwa kuanza kutekelezwa Mwaka wa Fedha
2026/2027”, alisema Mhe. Luswetula.
Akijibu swali la msingi kuhusu hatua zilizochukuliwa kudhibiti
mikopo hatarishi inayotolewa na baadhi ya taasisi zisizo
rasmi, Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali, BoT na wadau
wengine, imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti mikopo
hatarishi yenye riba kubwa kwa kuendelea kutoa elimu kwa
wananchi.
Alisema kuwa mikopo inapaswa kutolewa na watoa huduma
wenye leseni kutoka BoT kwa mujibu wa Sheria ya Benki na
Taasisi za Fedha ya Mwaka, 2006 pamoja na Sheria ya
Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka, 2018.
Hatua nyingine iliyochukuliwa ni pamoja na kuwatambua na
kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watoa mikopo
wasioidhinishwa ambapo programu 69 za mikopo ya kidigitali
zilizobainika kutoa mikopo bila leseni zilisitishwa na
programu 126 zilifungiwa.
Vilevile kutoa Mwongozo maalum kwa watoa huduma za
mikopo ya kidigitali ili kuhakikisha uwazi, uendeshaji wa
kimaadili, utoaji wa taarifa kamili kuhusu gharama za mikopo
pamoja na ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha.
Mhe. Luswetula alilitaja eneo lingine kuwa ni pamoja na
kuandaa rasimu ya kanuni za kusimamia mikopo ya kidigitali,
ambazo zinatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2026/27
ambapo Kanuni hizo zinalenga kuimarisha udhibiti wa
wakopeshaji wa kidijitali nchini Tanzania.
Aidha, Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali kupitia Wizara
ya Fedha, imekuja na programu ya elimu ya fedha ya mwaka
2020/2021 hadi 2025/2026 ikiwa ni mpango maalum wa
kutoa elimu kwa wananchi kwa makundi yote ambayo
inalenga kuwawezesha wananchi kupata uelewa, maarifa na
kuwajengea maarifa ya kusimamia mapato na matumizi na
kufanya maamuzi sahihi katika kutumia huduma rasmi za
kifedha.
Alisema kuwa Wizara ya Fedha kila mwaka
imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa
kuanzia mwaka 2021 na mwaka huu yamefanyika Jijini Tanga
kuanzia Januari 21, lengo likiwa wananchi kupata elimu ya
fedha.
Mhe. Luswetula alisema miongoni mwa Mikoa ambayo
maadhimisho hayo yamefanyika kuanzia mwaka 2021 ni
pamoja na Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na sasa
Tanga.
Hadi sasa takribani mikoa 16 imefikiwa na huduma ya elimu
ya Fedha na zaidi ya wananchi 64,000 wamefikiwa ikiwa ni
pamoja na wanawake 40,000 na wanaume 24,000 na
Halmashauri 94.
Mwisho.

0 Comments