Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Ndg. Sultan Said Suleiman, amezitaka kampuni zinazojihusisha na ujenzi wa nyumba za kisasa kuzingatia ujenzi wa nyumba za bei nafuu ili kuwawezesha Wazanzibari kubadili mfumo wa maisha na kuondokana na makazi ya nyumba za chini zilizojengwa bila kuzingatia mipango miji.
Ndg. Sultan ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Kampuni ya Karibu Group ulioongozwa na Bw. Sandro Giannubilo Beneduce, waliotembelea Ofisi za Shirika la Nyumba kwa lengo la kuwasilisha michoro na aina za ujenzi wa nyumba za kisasa kwa kutumia teknolojia mpya zinazohusisha mchanganyiko wa vyuma, saruji, jipsam na vifaa vingine vya kisasa.
Amesema mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha inakomesha ujenzi holela wa nyumba za makaazi kwa kuweka mazingira wezeshi ya ujenzi wa nyumba za kutosha katika maeneo mbalimbali ya visiwa hivyo, hatua itakayochangia kubadilisha taswira ya miji ya Zanzibar pamoja na kuwapatia wananchi makazi bora yenye huduma muhimu.
Mkurugenzi Sultan ameonesha kuvutiwa na miundo ya ujenzi na teknolojia iliyopendekezwa na kampuni hiyo, huku akiahidi ushirikiano wa karibu kutoka kwa wataalamu wa ujenzi na ukadiriaji wa Shirika la Nyumba ili kuhakikisha miradi hiyo inazingatia viwango vya ubora, uimara pamoja na maslahi mapana ya wananchi.
Hata hivyo, ameitaka Kampuni ya Karibu Group kuzingatia kwa makini uhakika wa kifedha na muda wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi, sambamba na kudumisha weledi na ubora wa hali ya juu katika kila hatua ya utekelezaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Biashara na Utawala wa Kampuni hiyo, Bw. Sandro Giannubilo Beneduce, amesema ujenzi wa nyumba hizo za kisasa utaambatana na uanzishaji wa kiwanda cha kutengeneza sehemu mbalimbali za nyumba, hatua itakayorahisisha ujenzi kwa haraka na kuhakikisha upatikanaji wa nyumba imara zinazodumu kwa muda mrefu.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Ndg. Muhaza Gharib Juma, pamoja na wataalamu wengine wa Shirika la Nyumba Zanzibar.

0 Comments