6/recent/ticker-posts

Zanzibar na U.A.E kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kiutendaji katika sekta za maji na umeme.

 


Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Nadir Abdullatif Al-Wardy, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mipango madhubuti ya kuhakikisha wananchi wanaondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika kipindi kifupi kijacho kwa kutumia mbinu mbadala za nishati.
Waziri Nadir ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) Zanzibar, Bw. Saleh Ahmed El-Hemiri, aliyefika Wizara hiyo Maisara kwa lengo la kusalimiana na kubadilishana mawazo kuhusu uimarishaji wa sekta ya maji, nishati na madini.
Amesema Wizara hiyo tayari imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali itakayowezesha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi, huku akieleza kuwa kikao hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ushirikiano baina ya Zanzibar na U.A.E kupitia kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kiutendaji katika sekta za maji na umeme.
“Tumeandaa mbinu mbadala kuanzia kwenye upatikanaji wa mchanga ambao tutautoa Tanzania Bara kwa ajili ya wawekezaji wakubwa. Kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara, tayari tumeingia mikataba mbalimbali ikiwemo ya nishati ya jua (Solar) na betri, sambamba na kuwa na mtambo maalum wa kuhifadhi umeme ambao tutauanza kuutumia hivi karibuni ili kuondokana na changamoto iliyopo,” amesema Waziri Nadir.
Aidha, ameongeza kuwa katika sekta ya maji, Serikali inaendelea na mipango ya kutandaza mabomba mapya katika mikoa na wilaya mbalimbali, pamoja na kufunga mashine mpya katika visima ili kuondokana na tatizo la maji machafu na yasiyo salama kwa matumizi ya wananchi, hatua inayolenga kuondoa kero za muda mrefu katika kipindi kifupi.
Kwa upande wake, Balozi Mdogo wa Umoja wa Falme za Kiarabu Zanzibar, Bw. Saleh Ahmed El-Hemiri, amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Madini katika nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo na ujuzi kwa watendaji ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi.
Amesema Zanzibar na U.A.E zina uhusiano wa muda mrefu wa kirafiki na kiudugu, hivyo wako tayari kufungua milango kwa wawekezaji na watu wenye nia njema kuja kuitembelea na kuwekeza Zanzibar kwa lengo la kuharakisha maendeleo.


Post a Comment

0 Comments