NA FAUZIA MUSSA
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ameitaka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kuhakikisha haki ya faragha zinalindwa kikamilifu, usalama wa taarifa binafsi unaimarishwa na zoezi la usajili wa hiari kwa taasisi zinazohusika na taarifa binafsi linafanikiwa.
Waziri Kairuki alitoa wito huo wakati akizungumza na watendaji wa Ofisi ya PDPC Upande wa Zanzibar, Amani Mjini Unguja, wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake.
Alisema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya matumizi mabaya ya taarifa zao binafsi, na kusisitiza umuhimu wa utekelezaji madhubuti wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
“Mnapaswa kutekeleza maagizo ya Serikali, na kuhakikisha ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria za taarifa binafsi unahusisha wadau wote wanaokusanya, kuhifadhi au kuchakata taarifa binafsi, ili tufikie azma ya kulinda faragha za watu,” alisema Waziri Kairuki.
Aidha, aliielekeza Tume hiyo kuanza maandalizi ya ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria za taarifa binafsi, kwa lengo la kuwahamasisha wadau kushirikiana kikamilifu na PDPC katika kufikia malengo ya kutunza na kulinda taarifa binafsi.
Waziri huyo alibainisha kuwa Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na PDPC, na kuiomba tume hiyo kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za faragha na umuhimu wa kulinda taarifa zao binafsi.
“Serikali inatambua juhudi zenu. Endeleeni kutoa elimu ili watu watambue faragha zao, na nyinyi tafuteni ujuzi zaidi wa ubobevu, kujipanga kwenye mafunzo na hata mashirikiano na nchi nyengine kama China na kwingineko, ili kupata uzoefu wa namna wenzetu wanavyokabiliana na masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi,” alisisitiza.
Pia aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha taasisi za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi zinajisajili Katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ili kutimiza matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.
Mapema, Waziri Kairuki alieleza kuridhishwa na utendaji wa Ofisi ya PDPC Zanzibar, akisema hatua zilizochukuliwa zinaonesha dhamira ya kweli ya kulinda haki za faragha za wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, alisema Tume hiyo imejipanga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na ukaguzi ili kuhakikisha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inazingatiwa ipasavyo.
“Tume inaendelea kuimarisha uwezo wa kitaalamu kwa watendaji wake, pamoja na kuendesha kampeni za elimu kwa umma, ili kila mdau awe na uelewa wa wajibu wake katika kulinda taarifa binafsi,” alisema Dkt. Mkilia.
Naye Mkurugenzi wa PDPC, Ofisi ya Zanzibar, Rehema Abdalla, alisema ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Sheria hiyo.
“Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi ofisi ya Zanzibar imejikita katika kuhakikisha taasisi zote zinazohusika na taarifa binafsi zinazingatia taratibu na viwango vilivyowekwa, ili kujisajili na kulinda faragha za watu,” alisema Rehema.
.jpg)
0 Comments