Mwaakilishi wa Jimbo la Mkoani, Mheshimiwa Khamis Amran Hijaz, amefanya kikao cha muhimu na chenye tija kubwa na viongozi wa dini wa Jimbo la Mkoani, Pemba, kwa lengo la kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya kuimarisha maadili, mshikamano wa kijamii na maendeleo ya kiroho katika jamii yetu.
Kikao hicho, kilichojaa hekima, heshima na moyo wa uzalendo, kimeakisi dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Mwaakilishi katika kushirikiana kwa karibu na viongozi wa dini kama nguzo muhimu ya malezi ya jamii yenye misingi imara ya maadili na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa ajenda kuu zilizojadiliwa ni mpango wa kudhamini mashindano makubwa ya kuhifadhi Qur’an Tukufu katika Jimbo la Mkoani, Pemba mpango wenye lengo la kuinua na kuhamasisha vijana na jamii kwa ujumla kuipenda, kuisoma, kuifahamu na kuihifadhi Qur’an, sambamba na kukuza vipaji vya kielimu na kiroho.
Mheshimiwa Khamis Amran Hijaz amesisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuzingatia misingi ya dini, maadili mema na mshikamano wa kijamii, na kwamba Serikali ya Jimbo itaendelea kushirikiana bega kwa bega na taasisi za dini katika kujenga jamii iliyo bora, yenye amani na heshima.



0 Comments