Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali inawajibu wa kuweka mazingira wezeshi kupitia sera madhubuti, ufadhili endelevu na ushirikiano utakao hakikisha changamoto kubwa ya ukosekanaji wa dawa ya insulini kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari inapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kushughulikia changamoto na vikwazo vya upatikanaji na usambazaji wa dawa ya Insulini uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema nchi nyingi duniani zenye kipato cha kati zinakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya watu wenye uhitaji wa dawa ya Insulini ambayo wanaikosa na kupelekea idadi ya wagonjwa wa kisukari kuongezeka siku hadi siku.
Mhe.Hemed amefahamisha kuwa jitihada za pamoja za kikanda zinahitajika ili kuhakikisha mahitaji ya upatikanaji wa dawa ya Insulini yanatimizwa ambapo kwa upande wa Tanzania itaendelea kuekeza katika kinga, uchunguzi wa mapema na huduma endelevu pamoja na kuunga mkono tafiti za Udhalishaji wa ndani wa dawa za Insulini.
Sambamba na hayo amesema serikali zina dhamira ya dhati ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari kwa kushirikiana na jamii, wadau wa Kikanda na Kimataifa pamoja na kubadilishana uzoefu na ubunifu ambao kwa kiasi kikubwa kutapunguza mzigo wa ugonjwa wa kisukari na kuboresha maisha ya watu wengi.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesema kupitia mkutano huo suluhisho la upatikanaji wa dawa za Insulini zenye ubora na unafuu litapatikana, minyororo ya ugawaji wa dawa yenye usawa, ubunifu katika matibabu na uimarishaji wa mifumo ya afya vitajadiliwa kwa upana wake na kwa ufanisi zaidi.
Aidha Makamu wa pili wa Rais Zanzibar ametoa wito kwa washiriki wote wa mkutano huo kushiriki kwa uwazi, kuwa wabunifu na kuzingatia suluhisho litakalotekeleza kwa vitendo uondoaji wa changamoto zinazowakabili wagonjwa wa kisukari Barani Afrika.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu ambae pia ni kaimu Waziri wa Afya wa Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Mpango wa Maendeleo endelevu wa mwaka 2050 umeweka viashiria muhimu vya utendaji ambavyo ni pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na maradhi yasiyo ya kuambukiza kutoka asilimia 4.9 kwa mwaka 2019 hadi asilimia 2.2 ifikapo 2050 jambo ambalo linahitaji Mifumo Imara ya Afya, mashirikiano na utayari wa kufikia malengo hayo.
Dkt. Mkuya amesema ili kuyafikia malengo hayo ni lazima kuwepo na mfumo Imara na endelevu wa huduma za afya ikiwemo upatikanaji wa Insulini yenye viwango na kwa wakati katika maeneo yote ya jamii.
Aidha amesema kumekuwa na changamoto ya usambazaji thabiti wa dawa ya Insulini hasa katika maeneo ya vijijini, gharama kubwa na uwezo mdogo wa familia nyingi wa kuweza kumudu dawa ya Insulini sambamba na utegemezi mkubwa wa kuagiza Insulini kutoka nchi za nje ya Bara la Afrika.
Hata hivyo, Dkt. Mkuya amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya upungufu wa wataalamu pamoja na uwelewa mdogo wa jamii kuhusu dalili za awali za kisukari aina ya kwanza na ya pili ambazo zinahitaji suluhisho la Kikanda na la Kimataifa kama ilivyosisistizwa katika Agenda ya Umoja wa Afrika mwaka 2063.
Kwa upande wake Dkt. Adelard Kakunze, Afisa Ufundi Mwandamizi wa Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Majeruhi na Afya ya Akili, Barani Afrika ( CDC) amesema lengo la mkutano huo ni kujadili kwa pamoja njia sahihi ya kuhakikisha dawa ya Insulini inapatikana kwa urahisi, ubora na unafuu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengi wanaoishi na ugonjwa wa kisukari.
Dkt. Kakunze amesema Afrika CDC itahakikisha kunakuwa na soko la uhakika na upatikanaji wa dawa za Insulini zenye ubora na kwa unafuu sambamba na kuangalia njia bora ya mifumo ya afya itakavyoweza kusaidia upatikanaji wa Insulini kwa usawa ili kuokoa maisha ya watu wanasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
Akimwakilisha Dkt. Alex Gasasira Mwakilishi Mkaazi nchini Tanzania kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni , Dkt. Alphoncina Nanai, Afisa wa Afya ya Umma wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka W.H.O amesema Shirika hilo limeweka mipango madhubuti ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa lengo la kudhibiti magonjwa hayo yasiendelee kuathiri watoto wadogo na wazee Barani Afrika.
Dkt. Nanai metoa wito kwa washiriki wa Mkutano huo kufanya kazi kwa pamoja hasa katika kupambana na upatikanaji wa huduma bora, dawa na matibabu ya ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza ikiwemo saratani na mengineyo.
Imetolewa na Kitengo Cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe ,…..03 / 02 / 2026
0 Comments