Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kufanyiwa mafunzo kwa viongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunawasaidia kufanikisha uendeshaji wa Bunge sambamba na kuimarisha ushirikiano baina ya wabunge na Serikali katika kusonga mbele kichumi, kisiasa na kijamii.
Ameyasem ahayo katika ufunguzi wa mafunzo ya kamati ya uongozi ya Wabunge,Tume ya Utumishi wa Wabunge na Makamu Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Bunge Tunguu Zanzibar.
Amesema Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imelipa uwezo Bunge kusimamia na kuishauri serikali kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya muda mrefu na mfupi, kutunga sheria zitakazosaidia utekelezaji wa masuala mbali mbali na kuridhia mikataba pamoja na kuuliza maswali yanayowagusa wananchi.
Kwa upande waTume ya Utumishi wa Bunge imepewa dhamana ya kusimamia utumishi wa bunge ikiwemo kusimamia Bajeti, rasilimali za Bunge na kuangalia maslahi ya watumishi wa Bunge na Wabunge.
Aidha, Mhe. Hemed amesema anaamini kuwa mafunzo hayo yatakuwa jukwaa muhimu ambalo litawapa fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza kwa pamoja na kujenga mtazamo wa pamoja kuhusu namna bora ya kuziendesha kamati zao kwa uweledi, ufanisi na kuwawezesha kuwa na Bunge la viwango.
Amewasisitiza viongozi hao juu ya umuhimu wa kushirikiana kwa karibu kati ya Bunge, Tume ya Utumishi wa Bunge na Serikali katika kuhakikisha kuwa majukumu ya Bunge yanatekelezwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria na kanuni ambazo huiwezesha serikali kufanya majukumu yake kwa ufanisi.
Nae Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Mussa Azzan Zungu (MB ) amesema katika mafunzo hayo wabunge watapata fursa ya kujifunza mambo mbali mbali yanayohusu utendaji wa kazi za bungu na mustakbali mzima wa uongozi kwa lengo la kuwatumikia viongozi na wananchi kwa ujumla.
Mhe.Spika Zungu amesema mafunzo hayo ya siku tano ambayo yameanzia Mkoani Dodoma yatajadili mada mbali mbali ikiwemo Madaraka, Majukumu, Mipaka na Utendaji Kazi wa Kamati na Uongozi wa Kimkakati Katika Uendeshaji Wa Shuhuli za Bunge.
Maada nyengine zitakazofundishwa na kujadiliwa katika mafunzo hayo ni Uratibu na Utekelezaji wa Shuhuli za Serikali katika Kamati za Bunge, Mahusiano na Changamoto, Haiba ya Viongozi na Itifaki ya Kidiplomasia Katika Utekelezaji wa Shuhuli za Kibunge na Kiserikali katika Ngazi ya Kitaifa na Kimataifa. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akiwa katika picha ya Pamoja na baadhi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya ufunguzi wa Mafunzo ya Kamati ya Uongozi ya Bunge, Tume ya Utumishi wa Wabunge na Makamu wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge yaliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge Tunguu Zanzibar.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )Leo tarehe ..16 / 02 / 2026
.jpg)

.jpg)
0 Comments