Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt.
Emmanuel Nchimbi akiagana na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju mara
baada ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria
nchini yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma,
leo tarehe 02 Februari 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt.
Emmanuel Nchimbi amesema kwa kutambua umuhimu wa
Mahakama katika ujenzi wa Taifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi
katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake
kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku
ya Sheria nchini yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania,
Tambukareli, Jijini Dodoma. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na
Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu,
kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama, na kusogeza huduma za utoaji haki
karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za
Mwanzo kwa Kata zote nchini zisizo na
Mahakama za Mwanzo.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwamba, uhuru wa Mahakama usitumike kama sehemu
ya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki. Amesema uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa
uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.
Makamu wa Rais amesema Mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia
utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa, na kuhakikisha kuwa
maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.
Ameongeza kwamba
Mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kwa
Kuendelea kulinda haki na misingi
ya Katiba, Kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa
kwa haraka na kwa haki, Kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa
kisheria wa nchi, Kukuza uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta
binafsi pamoja na Kudumisha amani na mshikamano wa Kitaifa, ambao ni msingi wa
maendeleo endelevu.
Pia amesema ni muhimu Mahakama, Kuzuia migogoro inayoweza
kuwa chanzo cha migawanyiko ya kijamii au kisiasa, Kuharakisha utekelezaji wa
sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri ya kisheria iliyo wazi na
thabiti, Kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimu sheria, haki na taasisi
za umma, Kuchangia katika mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka
pamoja na Kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa
kuwahakikishia ulinzi wa haki zao za kisheria.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewaasa viongozi,
wanasiasa, wanaharakati na wananchi mbalimbali kuheshimu tume iliyoundwa na
Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
29, 2025 kwa kuacha kuongelea masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria. Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo kufuatia
maombi ya Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniface
Mwabukusi ambaye aliomba Viongozi kuacha kuzungumzia suala hilo ambalo limekuwa
likiwaumiza wananchi.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju
amesema Mahakama inaendeleza na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli
za Mahakama ili kuimarisha ufanisi. Amesema kwa sasa Mahakama inajenga mfumo
unaotumia Akili Unde (AI) kwaajili ya kurekodi mwenendo wa kumbukumbu za
mashauri na hukumu Mahakamani.
Amesema katika mfumo huo, Jaji, Hakimu, Wakili na Shahidi
wanapozungumza mahakamani mfumo huo utatafsiri lugha iliyotumika na kuiandika
kwa lugha iliyokuwa imechaguliwa kuandika kwa wakati huo huo. Ameongeza kwamba
mfumo huo utakapoanza kutumika utaimarisha ufanisi wa utendaji wa Mahakama
kwani kuchukua kumbukumbu za mwenendo wa mashauri Mahakamani kwa kuandika kwa
mkono au kompyuta kunachelewesha na wakati mwingine kupotosha.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
02 Februari 2026
Dodoma.
.jpg)







0 Comments