Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametoa wito kwa Viongozi na Watendaji kuongeza kasi ya kuwatembelea na kuwakagua Wananchi, wakiwemo wenye mahitaji na maisha magumu, ili kuwasaidia na kuleta faraja kwa Jamii, hasa ndani ya Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Jumatatu Februari 23, 2026, akizungumza kwa nyakati tofauti na Wananchi wa Mikoa ya Kichama ya Kati na Kusini, alipowatembelea na kuwajulia-hali Wazee, Wagonjwa na Watu wanaokabiliwa na changamoto mbali mbali, wakiwemo pia Wafiwa, katika mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema, huo ni mwenendo mwema wa kheri, na utamaduni wa tangu asili, kwa Watu wa Visiwa vya Unguja na Pemba, na kwa dhamira pia ya kupeana faraja, hasa ufikapo Msimu wa Funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
"Tumeona huu ni mwenendo mwema tuliourithi kutoka kwa Wazee na Watangulizi wetu; na sisi tuuendeleze kwa kuwatembelea wenzetu, kwani kwa-kweli wenye uhitaji ni wengi, ila tusimamie lengo lile-lile la kusaidiana na kupeana faraja", amekumbusha.
Hivyo amesema, kutokana pia na ugumu wa maisha unaoendelea kuwakabili Wananchi wengi, ni wajibu kwa kila Kiongozi kujitoa na kuwaendea watu wengi zaidi, ili kuwakagua na kuwasaidia, huku akisisitiza kwamba; "kitendo hichi kinatupa fursa pia ya kuona hali ya watu na hali ya nchi yetu".
Wakitoa shukran kwa niaba ya Wazee na Wananchi waliopata fursa ya kujuliwa-hali, Mzee Haji Juma Haji wa Uzi-kisiwani, Jimbo la Tunguu na Bi Munira Khamis Zidi, wameutaja Mwenendo huo wa Viongozi kuwa ni jambo kubwa la faraja, hasa kwa Wananchi wanyonge wenye changamoto maishani.
Wazee hao wamemuomba Mwenyezi Mungu Azidi-kuwapa imani na azma njema Viongozi, waendelee kuwahurumia, kuwafikia na kuwasaidia Wananchi wanyonge.
Akiwa ziarani humo, Mheshimiwa Othman amepata fursa ya kuwajulia-hali Bi. Wache Abdallah Khamis, Mzee Haji Juma Haji, Bwana Suleiman Khamis Mwinyi, Bi. Munira Khamis Zidi na Bwana Juma Ramadhan Haji, wakaazi wa Kiboje, Uzi-Kisiwani, Charawe, Paje na Kaekuu, katika Majimbo ya Uzini, Tunguu, Chwaka, Paje na Makunduchi.
Katika Ziara hiyo, Mheshimiwa Othman ameambatana na Viongozi mbali mbali wa Majimbo ya Mkoa huo, wakiongozwa na Naibu Katibu wa Haki za Binaadamu wa ACT Wazalendo, Bi Pavu Abdalla Juma.
Mheshimiwa Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza Mstaafu wa Rais wa Zanzibar, ameanza Ziara hiyo ambayo huitekeleza kila mwaka, hasa ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Huo pia ni Muendelezo wa Mwenendo wa aliyekuwa Mtangulizi wake wa Nafasi hiyo, Almarhum Maalim Seif Sharif Hamad.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa
Februari 23, 2026.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

0 Comments