Vikwazo vitano visivyo vya kikodi kati ya kumi vilivyokuwa vikisababisha msongamano mkubwa wa malori na usumbufu kwa wafanyabiashara na wasafirishaji katika mpaka wa Tunduma/Nakonde, zimepatiwa ufumbuzi kupitia juhudi za pamoja za Serikali za Tanzania na Zambia. Hatua hiyo inatajwa kuwa chachu ya kuimarisha biashara za kimataifa katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha ujirani mwema kilichofanyika mpakani Tunduma na kuwakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka pande zote mbili, wakiongozwa na Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Mulambo Haimbe(Mb.)kwa upande wa Zambia.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Waziri Kombo ameeleza kuwa moja ya mafanikio makubwa ni kuridhia kwa serikali ya Zambia kuanza kutoa huduma kwa saa 24 kama ilivyo katika utaratibu wa Kituo cha Pamoja - One Stop Border Post (OSBP), hatua hii itakayopunguza kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa mizigo na msongamano wa magari ya mizigo katika eneo hilo.
Aidha, Zambia imekubali kutumia mashine ya kisasa ya mdaki (scanner) iliyotolewa na Serikali ya Tanzania ili kuongeza kasi na ufanisi katika ukaguzi wa mizigo, jambo litakalorahisisha uvukaji wa malori na kupunguza gharama za ucheleweshaji kwa wafanyabiashara.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kiteknolojia, pande hizo mbili pia zimekubaliana kusomanisha mifumo ya forodha ya TANCIS inayotumika Tanzania na ASYCUDA Plus inayotumika Zambia, ili kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa kwa haraka na kuongeza uwazi katika shughuli za mpakani.
Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza ushindani wa bandari na mipaka ya Tanzania, kuchochea biashara za kikanda na kimataifa, na kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili pamoja na ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa ujumla.



0 Comments