6/recent/ticker-posts

Mhe Riziki awataka Wakaazi wa Matemwe kuthamini mradi wa ujenzi wa viwanja vya michezo



Wilaya ya Kaskazini ‘A’

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma, amewataka wakaazi wa Kijini Matemwe kuupokea na kuuthamini mradi wa ujenzi wa viwanja vya michezo unaotekelezwa katika eneo hilo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Waziri huyo ametoa wito huo wakati wa ziara ya kutembelea eneo lililokabidhiwa kwa wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo katika Kijiji cha Kijini Matemwe, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja.

Amesema ujenzi wa miundombinu hiyo ni chachu ya ajira kwa vijana wa kijiji hicho, lakini akasisitiza kuwa wanafunzi wanaoendelea na masomo wanapaswa kuweka kipaumbele katika elimu yao badala ya kujihusisha na ajira hizo.

Aidha, amewaomba wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda na kuhakikisha usalama wa vifaa vya ujenzi wakati wa utekelezaji wa mradi huo, ili kukamilika kwa wakati na kufikia malengo ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Dkt. Raiziki ameeleza kuwa miundombinu hiyo iwapo itatuzwa na kulindwa itasaidia kudumu  kwa muda mrefu na kupelekea kukuza na kuibua vipaji vya vijana wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwakilishi waJimbo la Kijini Ambae pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Mhe. Badria Attai Masoud, amesema kuwa maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ni kuibadilisha Zanzibar kwa kujenga miundombinu bora ikiwemo barabara, masoko, skuli za ghorofa za msingi na sekondari, hospitali pamoja na viwanja vya michezo ili kuweka mazingira bora kwa wananchi wake

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Ndugu Makame Machano Haji, amewasihi wakaazi wa kijiji hicho kushirikiana vyema na wakandarasi katika kipindi chote cha ujenzi ili kufanikisha mradi huo kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Kaskazini ‘A’, Faki Zubeir Haji, ameishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo ambao utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo hilo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari – WHSUM


 

Post a Comment

0 Comments