Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema licha ya ugumu wa maisha unaowakabili Wananchi hapa Visiwani, wajibu uliopo kwa kila mmoja ni kupigania Haki na amani ya Nchi, hasa ndani ya Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Jumanne Februari 24, 2026, akiwasalimia Wananchi wa Mikoa ya Kichama ya Kaskazini A na B, kwa nyakati tofauti alipowatembelea na kuwajulia-hali Wazee, Wagonjwa na Watu wanaokabiliwa na matatizo mbali mbali, yakiwemo ya kiafya na Wasiojiweza, huko Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amefahamisha kuwa yeye na Viongozi wa Chama chake wameamua kuingia katika juhudi za kuleta Maridhiano ya Kisiasa na Upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kuwapunguzia machungu, Wananchi walio-wengi, kwa angalau kuwepo mazingira ya amani na utulivu wa kweli, hasa ndani ya Msimu huu wa Funga.
"Wazee wangu tunaelewa kwamba jana si leo; Ramadhani ya Mwaka-jana si ya Mwaka-huu, yaani tunaona hali inazidi kuwa ngumu kwa kila ambavyo siku zinakwenda", amesema.
Aidha amewabainishia Wananchi pamoja na Wafuasi wa Chama chake, huku akiahidi kuwajulisha baada ya kila hatua watakayofikia katika kupigania suluhu ya kisiasa Zanzibar akisema, "kama ambavyo tulitangulia-kusema katika Vikao vyetu vya hivi karibuni; na niwaambie tumesogea hatua zaidi, Inshaallah tutegemee kuila Sikukuu kwa furaha zaidi".
Aidha ameahidi kwamba Mapambano hayo ya kuitafuta haki na amani ya kweli nchini, sio kwamanufaa ya Viongozi na Chama chake, bali ni kwa mustakbali wa Zanzibar na watu wake kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman ameuzungumzia mtiririko na mwendelezo wa Ziara zake hizo kuwa ni Mwenendo Mwema ambao yeye na wenzake wameurithi kutoka kwa Wazee na Watangulizi, tangu asili na zama, akiwemo Mtangulizi wa Nafasi yake, Almarhum Maalim Seif Sharif Hamad.
Hivyo ametoa wito kwa Viiongozi kuuendeleza mwenendo huo na kuwafikia watu, hasa wananchi wanyonge, na kwa idadi kubwa zaidi, ili kuwasaidia kwa kadiri itakavyowezekana.
Wananchi hao wameeleza faraja yao kubwa waliyoipata kutokana na kufanyiwa Ziara na Kiongozi huyo, wakisema, pamoja na masaibu na shida walizonazo, bali wamejisikia kufarajika mno, huku wakiomba Utamaduni huo uendelee na uzidi kuenziwa.
"Sisi kwetu zaidi ni shukran kwako na Ujumbe wako Mheshimiwa; hii ni faraja sana kwetu, na tunazidi kumuomba Mungu Akupeni Nguvu na Ushindi, mzidi kutukumbuka na kutufikia kila inapobidi; kwa kweli tumejisikia faraja sana", amesema Bw. Ame Khamis Ame, wa Kilombero- Mfuruni.
Mheshimiwa Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza Mstaafu wa Rais wa Zanzibar, katika Ziara hiyo, amewajulia-hali Bi. Habiba Khamis Simba, Bi Raya Rashid Hemed, Mzee Mosi Makame Juma, Bi. Miza Juma Faki, Bi. Tatu Khamis Ali, Bi. Hamuyeji Uledi Makame, Bw. Juma Mtwana Haji, na Bw. Ame Khamis Ame, wote wakaazi wa Batini, Mahonda-Mahakamani, Mchangani, Kijagi-Skuli, Fukuchani-Mvuleni, Matemwe-Kusini Mwangaseni, Kikobweni na Kilombero-Mfuruni, katika Majimbo ya Bumbwini, Donge, Tumbatu, Nungwi, Kijini, Mkwajuni, Chaani na Mahonda.
Ziara hiyo imewajumuisha pia Viongozi na Watendaji Wakuu wa Kichama wa Majimbo na wa Mikoa hiyo, wakiwemo; Katibu wa Haki za Binaadamu wa ACT-Wazalendo, Bi Pavu Abdalla Juma, na Wenyeviti wa Mikoa ya kichama ya Kaskazini A na B, Ndugu Mcha Rajab Hajji na Bwana Silima Abdallah Juma.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa
Februari 24, 2026.




0 Comments