6/recent/ticker-posts

RAIS DKT. SAMIA AFANYA MAZUNGUMZO NA NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina Mohammed , tarehe 15 Februari, 2026 jijini Addis Ababa Ethiopia

Rais Dkt. Samia yupo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku nne ambapo, pamoja na shughuli nyingine, alishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika tarehe 14 na 15 Februari 2026.

………….

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Amina Mohammed, jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari S. Machumu, mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa katika maeneo ya maendeleo na diplomasia ya kimataifa.

Akinukuliwa katika taarifa hiyo, Bw. Machumu amesema Rais Dkt. Samia alieleza dhamira ya Tanzania katika kuendelea kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kiutawala, pamoja na kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan katika sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi ikiwemo afya, elimu, maji safi, usafi wa mazingira na kupunguza umaskini.

“Tanzania inaendelea kuthamini mchango wa Umoja wa Mataifa na taasisi zake katika jitihada za maendeleo, hususan katika ushirikiano wa kidiplomasia na msaada wa maendeleo unaotolewa katika sekta mbalimbali,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ikimnukuu Rais Dkt. Samia.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Dkt. Samia alionesha utayari wa Serikali kumpokea mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa aliyeomba kuja nchini kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.

Kwa upande wake, Bi. Amina Mohammed aliwasilisha salamu za Katibu Mkuu huyo na kueleza kuthamini ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa.

Akinukuliwa katika taarifa hiyo, amesema Tanzania imeendelea kuwa kinara wa amani barani Afrika na kupongeza juhudi za Rais Dkt. Samia katika kuimarisha mifumo ya taasisi pamoja na utatuzi wa changamoto kupitia mazungumzo na maridhiano.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mazungumzo hayo pia yaligusia mageuzi ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, ushiriki wa vijana katika maendeleo, pamoja na umuhimu wa kuimarisha uratibu kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

                


Post a Comment

0 Comments