6/recent/ticker-posts

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amuwakilisha Rais wa Zanzibar Mhe.Dkt.Hussein Mwinyi Mkutano Mkuu wa 17 wa ZNCC, Ukumbi wa Sheikh.Idrisa Abdulwakil Kikwajuni

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi  katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa kumi na saba (17) wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanya Biashara Zanzibar (ZNCC), uliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na azma yake ya kujenga uchumi shindani na jumuishi kwa kuifanya Zanzibar kuwa sehemu rafiki ya biashara na uwekezaji kwa kuweka miundombinu imara, Sera bora na huduma zenye ufanisi.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 17 wa Jumuia ya Kitaifa ya wafanyabiasha Zanzibar (ZNCC) katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Amesema katika kukuza biashara na uwekezaji nchini Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanya juhudi mbali mbali ikiwemo kuimarisha sera nzuri za uwekezaji, kuboresha miundombinu, kurahisisha taratibu za usajili wa biashara na uwekezaji na kulinda  haki maslahi ya wawekezaji.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa takwimu za serikali zinanaonesha kuwa jumla ya miradi ya uwekezaji 588, yenye thamani za dola za kimarekani Bilioni 6.9 imewekezwa Zanzibar na kuzalisha ajira 28,695 kwa wazawa.

Aidha, serikali imedhamiria kuchukua hatua madhubuti kama vile kuimarisha uendeshaji na ufanisi wa bandari, kuimarisha matumizi ya Tehama katika utoaji wa huduma, kuimarisha uhakika wa huduma ya nishati pamoja na kuweka  mazingira ya biashara na utendaji wa serikali.

Sambamba na hayo Serikali itahakikisha inaimarisha majadiliano ya kudumu katika sekta binafsi ambayo ni njia bora ya kujenga uaminifu, kupunguza migogoro ya kiutendaji na kuimaridha maendeleo ya biashara na uwekezaji Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anesema Serikali inatambua kuwa sekta binafsi ndio Injini ya uchumi hivyo itaendelea kuipa kipaombele ajenda ya kuboresha mazingira ya biashara yatakayowavutia wawekezaji na kuimarisha uzalishaji wa ndani.

Hata hivyo, ametoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kuwa mshirika wa serikali kwa kuwekeza katika uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa, kuzingatia ubora wa bidhaa na huduma, kuajiri na kuwajengea uwezo vijana kuweza kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati ili kuchangia maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wa  Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili ziweze kukua na kuchangia zaidi ukuaji wa uchumi ambao unahitaji kuwepo kwa amnai na mshikamano.

Nae Waziri wa kazi na uwekezaji ambae pia ni kaimu waziri wa Biashara na Maendeleo ya viwanda Zanzibar Mhe. SHARIF ALI SHARIF amesema Serikali inatambua kuwa Sekta binafsi ndio Injini ya Biasha nchini jambo linalochangia ukuwaji wa Uchumi na Uwekezaji Zanzibar.

Mhe. Sharif amefahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  inaendelea na utekelezaji wa sheria  ya Sekta binafsi ili kuhakikisha inaweka sawa mazingira ya biashara na uwekezaji nchi, sheria ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika kwake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya  Wafanyabiashara Zanzibar Ndugu. ALI AMOUR SULEIMAN amepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha miundominbu ya barabara, bandari pamoja na maboresho katika mifumo ya utoaji huduma serikalini hatua zilizoongeza ufanisi na kuimarisha sekta ya Uwekezaji.

Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo bado Jumuiya hio inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kukosekana kwa umeme wa uhakika na Kuzorota kwa ufanisi wa Bandari za Zanzibar.

Mwenyekiti Ali amesema kukatika kwa umeme mara kwa mara kunasababisha hasara katika viwanda, biashara za chakula, sekta ya utalii na huduma za teknolojia ambapo (ZNCC) wameshauri kuongezeka kwa huduma ya uzalishaji wa umeme, kuboresha miundombinu ya gredi na kuimarisha mawasiliano ya haraka kati ya watendaji wa Shirika la Umeme, Sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wa sekta ya bandari inakabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji wa mizigo, uratibu usioridhisha, gharama na tozo kubwa kwa wafanyabiashara ambapo wameiomba serikali kuimarishwa kwa mifumo ya kidijitali katika uendeshaji wa bandari, kuanzishwa kwa kituo cha ONE STOP CENTER sambamba na kuboreshwa miundombinu ya vifaa vya Bandarini.

Akizungumza kwa niaba wa wadhamini wa Mkutano wa 17 wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiasha Zanzibar (ZNCC ), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ ) ndugu Hamad Hamad amesema kutanuka kwa huduma mbali mbali za kibenki kunapelekea kuimarika zaidi kwa uchumi wa Taifa na kupunguwa kwa changamoto za upatikanaji wa  huduma za kifedha katika maeneo mbali mbali mjini na vijijini.

Amesema Benki ya watu wa Zanzibar imekuwa ikitoa huduma mbali mbali za kifedha kwa lengo la kukidhi mahitaji ya Wafanyabiasha na wananchi kwa ujumla ambapo amewashukuru Wafanyabiashara kwa kuendelea  kufanyakazi na PBZ, kuishauri na kutoa maoni yao kwa lengo la kuimarisha zaidi utendaji kazi wa Benki hio. 






Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe  ..16 / 02 / 2026.

Post a Comment

0 Comments