Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dkt. Habiba Hassan Omar, amesema ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau wa sekta ya viwanda ni njia muhimu ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo na hivyo kuinua uchumi wa taifa.
Dkt. Habiba aliyasema hayo katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Viwanda uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alieleza kuwa mkutano huo una lengo la kuweka mwelekeo sahihi wa maendeleo ya sekta ya viwanda na kuleta matokeo chanya kwa taifa.
Amefafanua kuwa Serikali ipo tayari kuendeleza mashirikiano na wadau wa sekta hiyo, akisisitiza kuwa viwanda vina mchango mkubwa katika kuzalisha ajira kwa vijana na kuongeza pato la taifa.
Aidha, alikiri kuwepo kwa changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo, lakini akasisitiza kuwa matarajio ya ukuaji ni makubwa kwa manufaa ya nchi na wananchi wake. Alieleza kuwa ipo haja ya kuifungua zaidi sekta hiyo ili kuongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana Zanzibar na hivyo kukuza uchumi.
“Ingawa kuna changamoto nyingi, Serikali inaendelea kuzitatua ikiwemo changamoto ya umeme na huduma za bandari,” alisisitiza Dkt. Habiba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazalishaji Zanzibar (MCZ), Ahmed Yussuf Baalawy, amesema ipo haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kukuza viwanda ili kupata soko la uhakika kwa bidhaa za ndani. Alipendekeza kuwepo kwa udhibiti maalum wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ili kulinda na kukuza uzalishaji wa ndani.
Naye Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Uzalishaji wa Chakula cha Paka, Kassim Said Moh’d, alieleza matumaini yake kuwa changamoto zilizowasilishwa, ikiwemo suala la kodi na tozo zinazodhoofisha uzalishaji, zitafanyiwa kazi ili kuimarisha sekta hiyo.
Katika mkutano huo wa siku moja, wadau walijadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha sekta ya viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.



0 Comments