6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAJENGA SKULI YA KISASA JANG'OMBE KUPUNGUZA MIKONDO MWILI




NA FAUZIA MUSSA

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya elimu kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wote wa sekondari na msingi wanaingia mkondo mmoja, hatua itakayoongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.
Waziri Lela aliyasema hayo wakati akikabidhi rasmi eneo la ujenzi wa Skuli mpya ya Jan’gombe (G+3) katika hafla iliyofanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 100 za uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane, Kipindi cha Pili.
Alieleza kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika kupunguza tatizo la mikondo miwili, huku zikibakia asilimia 20 ya skuli za sekondari na asilimia 30 ya skuli za msingi ambazo bado zinaingia mikondo miwili kwa siku.
“Tumefanya kazi kubwa na sasa tumebakisha asilimia ndogo sana. Lengo letu ni kumaliza kabisa mikondo miwili ili wanafunzi wetu wapate muda wa kutosha darasani, kwenda madrasa na nafasi ya kushiriki shughuli nyengine kama michezo ,” alisema Lela
Alibainisha kuwa ujenzi wa skuli hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya elimu Unguja na Pemba, ili kuwa na mazingira bora ya kujifunzia yanayokwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya kielimu na kiteknolojia.
Katika kuhimiza uwajibikaji, Waziri Lela aliitaka Kamati ya Usimamizi wa Mradi kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Aidha, aliwataka wakandarasi kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wazawa, hususan katika kazi zisizohitaji ujuzi maalum.
“Hatutaki vijana wawe watazamaji katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao. Washiriki kikamilifu, kwani wao ndio watakaokuwa walinzi wa miundombinu hii,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khamis Abdulla Said, alisema skuli hiyo ya kisasa itakuwa na madarasa 38, maabara za sayansi, chumba cha kompyuta na maktaba, pamoja na miundombinu mingine muhimu itakayowezesha utoaji wa elimu bora.
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kununua samani na vifaa vya kisasa ikiwemo madawati, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya intaneti ya uhakika, ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa kutumia teknolojia na kwenda sambamba na mapinduzi ya kidigitali.
Alifahamisha kuwa mradi huo unagharamiwa kwa asilimia 100 na Benki ya Dunia, na unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni nane hadi kukamilika kwake.
Aidha, alieleza kuwa ujenzi wa skuli za aina hiyo utafanyika katika wilaya zote za Unguja na Pemba.
Akizungumzia kuhusu ujenzi huo, Mshauri Elekezi wa Mradi, Mhandisi Valence Ngashweki, alisema skuli hiyo itakuwa na ghorofa tatu (G+3), ambapo mkataba wa ujenzi ulisainiwa Januari 5, 2026 na unatarajiwa kukamilika Januari 2027.
Alisema matarajio yao ni kuukabidhi mradi huo kabla ya muda uliopangwa, akibainisha kuwa hadi sasa hakuna changamoto inayokwamisha utekelezaji wake.
Naye Mkandarasi wa mradi huo, Fakihi Abdalla Pandu, aliahidi kuutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaostahili, akieleza kuwa maandalizi yalianza mara tu baada ya kusainiwa kwa mkataba.
Mwakilishi wa Jimbo la Jan’gombe, Ali Abdulghulam Hussein, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake za kuwaletea wananchi maendeleo, huku akiwaomba walimu wa skuli hiyo kuwa wavumilivu katika kipindi chote cha ujenzi.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali inayoongozwa na Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, inayolenga kuimarisha sekta ya elimu kama nguzo kuu ya maendeleo ya rasilimali watu na ustawi wa Taifa.


 

Post a Comment

0 Comments