6/recent/ticker-posts

Taasisi ya Indian Institute of Technology-Madras (IIT-M) yasifu jitihada za Serikali kuimarisha elimu na ubunifu

Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Dkt Aboud Suleiman Jumbe pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdullah Said, walikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Taasisi ya Indian Institute of Technology-Madras (IIT-M) kuhusiana na fursa mbali mbali za kuzisaidia Sekta za Elimu na Utalii katika ukondoishaji wa mafunzo, uundaji na matumizi ya mifumo ya kidijitali ikiwemo Akili Bandia au Artificial Intelligence katika sekta.
Professor Raghunathan Rengaswamy, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Chuo cha IITM Zanzibar ambaye pia ni Dean - Global Engagement wa Chuo cha IITM, alisifu juhudi zinazochukuliwa na Zanzibar katika kuimarisha elimu na ubunifu katika maendeleo ya Kidijitali nchini, huku akigusia nafasi maalum ya Sekta ya Utalii katika kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuboresha ufanisi, mapato na huduma za Utalii hapa Zanzibar.
Akifuatana na Professor Preethi Aghalayam, Director-in-Charge, IITM Zanzibar, Profesa Rengaswamy alisema kuwa wakati umefika sasa kwa Zanzibar na hususan Sekta ya Utalii, kuchangamkia fursa mbali mbali zinazotolewa na Chuo cha IITM katika kutoa elimu ya kidijitali na AI kwa faida ya wananchi wote ikiwemo Sekta mbali mbali za uchumi na maendeleo hapa Zanzibar, na kwamba IITM Zanzibar ipo tayari kuisaidia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale katika uundaji na matumizi ya mifumo ya kidijitali yatakayoimarisha sekta hiyo.
Wizara tayari imeanzisha mifumo ya kidigatili na AI kama vile Mfumo wa Jozani AI Model, Mifumo ya kidijitali ya uimarishaji wa ukusanyaji mapato, pamoja na mchakato unaoendelea wa kutengeneza mtandao unaojumuisha mitandao ya waongoza safari za watalii wanaokuja Zanzibar.
Hivi karibuni, Chuo cha IITM kilitoa Semina ya Mafunzo Mifumo ya Kidijitali na AI kwa Makatibu Wakuu na kuazimia kuendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa watendaji wengine wa Sekta ya Umma na Binafsi kulingana na mahitaji na vipaumbele vya kisekta, sambamba na dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza, ya kuhakikisha Sekta za Serikali kutumia mifumo ya kidijitali kuongeza Ufanisi.


 

Post a Comment

0 Comments