Wajumbe wa Mkutano wa 48 wa Baraza la Mawaziri Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa 48 wa Baraza la Mawaziri Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia Februari 11-12, 2026. Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.shimiwa Mahmoud Thabit Kombo (Mb).
Mkutano huo unawakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na viongozi waandamizi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kujadili masuala muhimu ya maendeleo, usalama, ushirikiano wa kikanda na utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mhe. Mahmoud Youssouf Ali, amesisitiza umuhimu wa mageuzi ya Taasisi na umuhimu wa amani na maendeleo barani Afrika kuelekea Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU.
Amesema kuwa, Mageuzi yanaendelea chini ya Mpango wa 2024–2028 na kubainisha mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha muundo wa amani na usalama, kuhakikisha ufadhili endelevu, pamoja na kuimarisha taasisi za Umoja huo.
Mwenyekiti huyo ameishukuru Jamhuri ya Angola kwa uongozi wake wa Baraza la Utendaji, huku Angola ikiwa ni Mwenyekiti wa Umoja huo anayemaliza muda wake.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Mhe. Gedion Timothewos, ameeleza kuwa mabadiliko yanayoendelea katika siasa za kimataifa yanazidi kudhoofisha misingi ya ushirikiano wa kimataifa na mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.
Amebainisha kuongezeka kwa ushindani wa kimataifa katika ubora wa teknolojia, udhibiti wa madini muhimu ya kimkakati, pamoja na umiliki na ushawishi katika njia kuu za kimkakati za usafirishaji na usambazaji bidhaa kama miongoni mwa changamoto hizo.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi ya Afrika (UNECA) Mhe.Clever Gatete ameongelea masuala muhimu ya kuzingatiwa na Umoja wa Afrika ili kuwa na maendeleo na ushindani thabiti.
Masuala hayo ni pamoja na kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa nchi wanachama, kuunganisha miundombinu ya uzalishaji, kuongeza thamani ya madini na mazao, kuimarisha soko huru barabi Afrika na kutumia maarifa na teknolojia ya sasa.
Mkutano huo wa ngazi ya juu wa mawaziri ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Kikao cha 39 cha Kawaida cha Wakuu wa Nchi na Serikali
0 Comments