6/recent/ticker-posts

Mhe Hemed akutana na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi



 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi uliofika ofisini kwake Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar kwa ajili yakujitambulisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema msingi mkubwa ya wiazara ya mambo ya Ndani ya Nchi ni kuhakikisha inalinda wananchi na mali zao pamoja na kutenda haki kwa raia wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania.

 

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi uliofika ofisini kwake Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar kwa ajili yakujitambulisha.

 

Amesema suala la usalama wa raia na mali zao ni jambo muhimu  katika kuimarisha shuhuli mbali mbali zikiwemo za kisiasa,  kiuchumi na kijamii ambapo kwa kuzingatia umuhimu huo Jeshi  la polisi  na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama wana wajibu wa kuhakikisha uwepo wa Amani na Utulivu  nchini kwa nyakati zote.

 

Mhe. Hemed amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia  katiba , sheria na miongozo mbali mmbali ili kuwa na utawala bora katika kuwahudumia wananchi wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania.

 

Aidha, makamu wa pili wa rais wa Zanzibar amesisistiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutumia teknologia katika utendaji wao wa kazi za kila siku

 

Sambamba na hayo, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano na miongozo stahiki ili kuhakikisha wanatekeleza maagizo yote yanayotolewa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulizi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan kwa yale yote aliyokusudia kuyatimiza.

 

Kwa upande wake Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.  PATROBAS PASCAL KATAMBI ( MB ) amesema dhamana waliyopewa ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao ni kubwa hata hivyo ameahidi  kufanya   kazi kwa Uweledi, Uaminifu na kwa kufuata misingi ya Kikatiba, Kisheria, Taratibu, Kanuni na miongozo mbali mbali.

 

Waziri KATAMBI amesema watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi watafanya kazi kwa bidii na nidhamu kwa kuhakikisha wanailinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuulinda Muungano wa Tanzania na kuzilinda Tunu za Taifa ili kuendelea kuiletea heshima Tanzania ndani na nje ya mipaka yake.

 

Amewapongeza viongozi wakuu wa nchi kwa kuliongoza Taifa kwa kufuata misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, misingi ya haki za binaadamu na misingi ya kutoa ustawi bora wa wananchi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 

 Katika ziara hio Mhe, KATAMBI ameambatana na  Mhe. AYOUB MOHAMMED MAHMOUD Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Ndugu ALLY  SENGA GUGU Katibu Mkuu na Ndugu MIRIYAM PEREELE MMBANGA Mkurugenzi wa Diviseni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi.  

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe 11 / 02 / 2026

Post a Comment

0 Comments